Makamu wa Rais asisitiza kuhusu malezi na maadili kwa vijana

ARUSHA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi kutambua jukumu walilonalo la malezi ya kimaadili kwa vijana ili kukabiliana na changamoto ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati aliposhiriki Ibada ya kuwekwa Wakfu na Kuingizwa kazini kwa Askofu Mteule Dkt. Abel Godson Mollel na msaidizi wake Mchungaji Lareiton Lukumay iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Kimandolu mkoani Arusha.

Amesema pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya vijana bado muitikio wa vijana hao katika nyumba za ibada ni mdogo hali inayopelekea kukosa mafundisho ya dini ambayo yangewawezesha kuwa na maadili na matumizi bora ya mitandao ya kijamii.

Aidha, Makamu wa Rais amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wote itasimamia na kulinda katiba ya nchi ikiwemo haki ya kuabudu kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Amesema serikali itahakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na kupata huduma bora za kijamii pamoja na kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta zote ambayo ikikamililika itachangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa Taifa.

Makamu wa Rais amewasihi viongozi wote wa dini nchini kusaidia kutoa hamasa kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.

Amesema Serikali inaahidi kufanya jitihada za kuweka mazingira ya haki na wezeshi ili wananchi waweze kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu.

Halikdahalika amesema Serikali inajivunia ushirikiano mzuri uliopo kati yake na taasisi za dini ambao umedumu kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali na inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa katika utoaji wa huduma za jamii, hususan elimu, afya na maji.

Ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha inatatua changamoto zinazokwamisha ubia baina ya serikali na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center haraka iwezekavyo.

Makamu wa Rais amewahimiza viongozi wa dini, waumini na watanzania kwa ujumla kuendelea kulinda na kudumisha amani, umoja na uhuru.

Aidha amewasihi viongozi wa dini kuendelea kupaza sauti kuhamasisha ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika nchi kwa kukemea ukataji na uchomaji hovyo wa misitu na uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali.

Amesema ni muhimu kuwahimiza waamini na wananchi wote kuheshimu na kuzingatia matumizi bora ya ardhi hususani maeneo ya kilimo, mifugo na vyanzo vya maji.

Makamu wa Rais amewapongeza Askofu Dkt. Abel Godson Mollel na Msaidizi wake Mch. Lareiton Lukumay kwa kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini na kuwasihi waamini wa Dayosisi hiyo na Wakristo wote kwa ujumla kutambua wajibu waliyonao kwa Viongozi wa kiroho.

Amewaasa waamini kumpa ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na kumpenda, kumtii, kumtia moyo na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Askofu Dkt. Abel Mollel ili aweze kutenda vema kazi yake.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt. Abel Mollel amesema Dayosisi hiyo itaendelea kushirikiana vema na serikali katika kutoa huduma za kijamii kama vile elimu na Afya.

Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano na Kanisa ambao umewezesha kufanikisha shughuli mbalimbali ikiwemio kupanda miti zaidi ya laki tatu katika mkoa huo.

Akizungumza katika ibada hiyo Askofu anayemaliza muda wake katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt. Solomon Massangwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mtetezi mzuri wa Katiba ya nchi.

Amesema,hatua ya kuruhusu vyama kufanya maandamano inaonesha hatua za wazi kulinda haki zilizopo katika katiba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news