Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato kuwa kituo cha umahiri matibabu ya moyo

GEITA-Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato kuwa kituo cha umahiri wa matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi wa moyo.

Ni katika ukanda huo wa ziwa ambao utarahisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.
Waziri wa Afya,Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo Machi 16, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Stanslaus Nyongo kukagua miradi ya ujenzi wa jengo la wodi la ghorofa mbili.

Sambamba na jengo la kutakasia vifaa yanayojengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.

“Kanda ya Ziwa ina watu karibu milioni 22, hivyo tukaona kuna haja ya kuwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda nyingine katika ukanda huu wa ziwa na ianze kutoa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi wa moyo katika ukanda huo wa ziwa ili waweze kusaidiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando,” amesema Waziri Ummy.

Amesema, kesi za magonjwa ya moyo za watu wa Kanda ya Ziwa (Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kagera pamoja na Kigoma) wanataka ziishie Chato ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo karibu na wananchi wa kanda ya ziwa pamoja na kupunguza msongamano wa wagonjwa wa moyo JKCI jijini Dar es Salaam.

“Tunataka tuwahakikishie Watanzania hakuna kilichosimama, toka Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeingia madarakani tumeendelea kutoa fedha, tutaendelea kuipa umuhimu wa kipekee Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato ili watu wote wenye changamoto ya Moyo na magonjwa mengine waishie Chato,”amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kutembelea katika hospitali hiyo na kupitisha fedha ambazo zinaendelea kusaidia katika ukamilishaji wa majengo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.

Aidha,Waziri Ummy amekamilisha ziara yake katika Kanda ya Ziwa ambapo alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekotoure), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news