TANAPA ilivyoboresha maisha ya wananchi, kupaisha pato la Taifa

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kurekodi mafanikio makubwa kupitia ongezeko la watalii na mapato ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan huku wananchi wakiendelea kuneemeka kupitia miradi.

TANAPA ni taasisi ya umma ambayo ipo chini ha Wizara ya Maliasili na Utalii huku ikisimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa.

Maeneo ya Hifadhi za Taifa yanawakilisha kiwango cha juu kabisa cha uhifadhi wa wanyamapori nchini (highest conservation status of wildlife) ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoruhusiwa kufanyika.

Hadi sasa shirika linasimamia hifadhi za Taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na asilimia 10.2 ya eneo lote la nchi.
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji ameyasema hayo Machi 21, 2024 katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

"Awali ya yote napenda kutumia fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia kuwepo hapa siku ya leo. Pili nitoe pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi mahiri na juhudi kubwa anazozifanya katika kuimarisha na kukuza sekta ya uhifadhi na utalii nchini.

"Katika kipindi chake cha uongozi wa nchi kwa miaka hii mitatu. Pia, nitumie nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

"Vilevile, nitoe pongezi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuratibu programu hii muhimu ya kueleza kwa umma mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."

Kamishna Kuji anasema,mafanikio ya sasa ndani ya TANAPA msingi wake mkuu ni jitihada za makusudi zinazoendelea kufanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Juhudi ambazo amesema,zinaambatana na ushiriki wake wa moja kwa moja kwenye kukuza sekta ya uhifadhi wa wanyamapori na utalii ikiwemo ushiriki wake kwenye filamu maarufu ijulikanayo kama “Tanzania: The Royal Tour”.

"Filamu hii imeleta chachu kubwa katika ukuaji wa utalii hapa nchini. Tunampongeza sana Mhe. Rais kwa mchango wake huu katika sekta ya uhifadhi na utalii hapa nchini pamoja na kuendelea kuelekeza fedha katika sekta ya uhifadhi na utalii."

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Kamishna huyo amesema, Filamu ya Tanzania, The Royal Tour ilifungua milango ya utalii na fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa hasa baada ya nchi kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19.

"Katika Hifadhi za Taifa kumekuwa na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa mwaka hadi mwaka.

"Mfano katika mwaka 2018/2019 jumla ya watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa walikuwa watalii 1,452,345 ikihusisha watalii wa ndani (719,172) na nje (733,173)."

Kamishna Kuji, amesema idadi hiyo ilianza kupungua mwanzoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga ya UVIKO-19 na kusababisha idadi ya wageni kupungua hadi kufikia watalii 485,827 katika mwaka 2020/2021.

"Kufuatia anguko hili la utalii, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua mbalimbali katika kurejesha hali ya utalii kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo kutengenezwa kwa miongozo maalum (Standard Operating procedures - SOPs) ya kupokea na kuhudumia watalii, na pia kuruhusu upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19.

"Hili lilienda sambamba na utangazaji mahiri wa vivutio vyetu kupitia filamu ya Tanzania:The Royal Tour iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa 2022."

Amesema, kutokana na jitihada hizo za Mhe. Rais, mnamo mwaka 2021/2022 idadi ya watalii ilianza kupanda na kufikia watalii 997,873.

Kamishna Kuji amesema, hali ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda ambapo mwaka 2022/2023 idadi ya watalii waliongezeka na kufikia 1,670,437.

Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 idadi ya watalii 1,514,726 (wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183) wametembelea hifadhi za Taifa sawa na ongezeko la asilimia tano ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 (wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676) katika kipindi husika.

Pia amesema, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667).

Vilevile,Kamishna Kuji amesema, katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024.

"Ongezeko hili limechangia ongezeko la mapato.Katika kipindi cha miaka mitatu, kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023) sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94."

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024), Kamishna Kuji amesema, shirika limekusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811,506 mpaka Machi, 2024.

"Kiasi hiki (shilingi bilioni 340) ni ongezeko la shilingi 44,634,296,959 ambayo ni sawa na asilimia 15. Shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha shilingi 382,307,977,497 hadi Juni 2024."

Kamishna Kuji amesema, mapato haya ya sasa yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO-19 ambayo yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika shirika.

Amesema, ongezeko hili la watalii na mapato linaenda sambamba na malengo ya Ilani ya Chama Chama Cha Mapinduzi ya 2020 hadi 2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini kufikia milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani Bilioni 6 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Pia amesema, kumekuwepo na kuchipuka kwa masoko mapya ya utalii yenye idadi kubwa ya watalii ambapo inatoa uhakika wa kuendelea kupokea watalii wengi kuja kutembelea Hifadhi za Taifa.

"Masoko haya mapya ni pamoja na China, Urusi, Ukraine, Poland, Jamhuri ya Czech na Israeli.

"Na TANAPA imefanikiwa kupata tuzo ijulikanayo kama “Best Practice Award” ambayo hutolewa kila mwaka na taasisi ya “European Society for Quality Research - ESQR”.

"Tuzo hii ya utoaji wa huduma bora kimataifa
hutolewa na taasisi hiyo baada ya kutambua taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za ubora wa viwango vya hali ya juu kimataifa."

Kamishba Kuji ameongeza kuwa, pia TANAPA imeendelea kupata tuzo zinazotolewa na taasisi ya ESQR kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.

Amesema,kati ya hizo tuzo za miaka mitatu mfululizo zimepatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango cha “Platinum category” mwaka 2021, “Gold category” mwaka 2022 na “Diamond category” mwaka 2023.

"Hifadhi ya Taifa Serengeti imepata tuzo itolewayo na shirika la “World Travel Awards (WTA)” ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo (2019 hadi 2023).

"Tuzo tatu kati ya hizo tano zimepatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita (tuzo za mwaka 2021 hadi 2023)."

Ameongeza kuwa, Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kilimanjaro zilipata tuzo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2021 na 2022 ya kuwa vituo vyenye mvuto katika utalii (best of the best outdoor enthusiasts).

Tuzo hizi hutolewa na jukwaa la kimataifa lijulikanalo kwa jina la “Trip Advisor”.

Pia, kampuni ya Explore Worldwide yenye makao yake makuu nchini Uingereza mwaka huu 2024 imeutambua Mlima Kilimanjaro kuwa namba moja ya Alama za Asili za kudumu na zinazokumbukwa zaidi ulimwenguni (World’s topmost unforgettable natural landmarks).

"Tuzo hizi zimeliongezea shirika kuaminiwa na wateja mbalimbali na kutoa uhakika kwao kuhusu aina ya huduma zitolewazo, kutambulika zaidi na kuongeza idadi ya watalii pamoja na kutoa uhakika kwa watalii na wadau wa utalii kuhusu ubora wa hifadhi."

Mbali na hayo, Kamishna Kuji amesema, kumekuwa na ongezeko la maeneo ya malazi na wawekezaji katika Hifadhi za Taifa.

Amesema,uwekezaji umelenga kuboresha huduma za malazi katika Loji, Kambi za Kudumu (Permanent Tented Camps - PTC), Kambi za Muda (Seasonal Camps), Kambi za Jumuiya (Public Camp Sites), Mabanda (cottages) na Hosteli.

"Uwekezaji huu umeongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda 5,755 mwaka 2021 hadi vitanda 10,094 mwaka 2024. Hata hivyo, ujenzi wa malazi unaendelea wenye uwezo wa vitanda 1,148 ambapo ukikamilika kutakuwa na vitanda 11,242."

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji ameyasema hayo leo Machi 21, 2024 katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni taasisi ya umma ambayo ipo chini ha Wizara ya Maliasili na Utalii, lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa.

Maeneo ya Hifadhi za Taifa yanawakilisha kiwango cha juu kabisa cha uhifadhi wa wanyamapori nchini (highest conservation status of wildlife) ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoruhusiwa kufanyika.

Hadi sasa Shirika linasimamia hifadhi za Taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na asilimia 10.2 ya eneo lote la nchi.

Vile vile, Kamishna Kuji amesema,kumekuwepo na ongezeko la bidhaa za utalii katika maeneo mengine ambayo awali hayakuwa na bidhaa husika.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni kuongezeka kwa wigo wa shughuli za utalii wa puto kutoka kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa Hifadhi ya Mikumi.

"Utalii wa faru katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, utalii wa baiskeli katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha.

"Nyingine ni utalii wa michezo na burudani katika Hifadhi ya Taifa Serengeti mchezo wa tennis na Hifadhi ya Taifa Mikumi mpira wa miguu, pete na kikapu."

Amesema, pia kuna ongezeko kwa mbio za Marathon katika maeneo ya ndani na pembezoni mwa hifadhi za Taifa ambapo zimekuwa zikivutia washiriki wengi na wakati huo huo kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo husika.

"Hifadhi zilizofanikiwa kuratibu mbio za Marathoni ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Arusha, Mkomazi, Ruaha, Katavi, Mahale, Gombe, Burigi- Chato na Kilimanjaro."

Wakati huo huo, Kamishna huyo amesema,mwaka 2018 TANAPA iliingia katika mchakato wa kutambuliwa na Shirika la Viwango Duniani ili kujijengea kuaminiwa na wateja.

Amesema, kutambuliwa kwa TANAPA mwaka 2021 na Mfumo wa Utoaji wa Huduma kwa kiwango cha Kimataifa (ISO) kumewezesha wateja kuamini na kuchagua huduma zinazotolewa na shirika ikiwemo hifadhi zake hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.

"Katika miaka mitatu, shirika limeendelea kutekeleza shughuli za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha ubora cha ISO 9001:2015 kinachohusu utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Miundombinu

Kamishna Kuji amesema, TANAPA imeendelea kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kukamilisha ujenzi wa lango la kisasa la Naabi.

Ni lango lenye uwezo wa kupokea zaidi ya magari 600 na wastani wa wageni zaidi ya 1,500 kwa siku.

Katika kipindi cha miaka mitatu TANAPA pia imeweza kujenga malango mapya 10 na ya kisasa katika Hifadhi za Taifa Tarangire (2), Mkomazi (3), Serengeti (2) na Nyerere (3).

"TANAPA imekuwa ikishinda tuzo za uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa kufuata viwango vya kimataifa kwa upande wa taasisi za umma zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA)."

Anasema, shirika limekuwa mshindi wa pili wa tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu za mwaka 2022 katika kundi la taasisi za kiserikali zinazotumia mfumo wa IPSASs (2nd winner in the government agencies category (users of IPSASs) for the best presented financial statements award for the year 2022).

"Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Ujerumani (KfW), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeendelea kuboresha (kujenga na kukarabati) miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vilivyopo katika Hifadhi za Taifa.


"Shirika lina mtandao wa barabara ambao umeongezeka kutoka urefu wa kilometa 7,638 mwaka 2021 na kufikia urefu wa kilometa 16,471 mwaka 2024."

Kamishna Kuji anasema, kazi nyingine za miundombinu zilizofanyika ni pamoja na kukarabati wastani wa kilometa 3,938 za barabara.

Pia,kutengeneza njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 334 ikiwemo ujenzi wa madaraja 14 na vivuko 399.

"Na kukarabati viwanja vya ndege (Airstrips) 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) na viungio vyake pamoja na maegesho ya ndege kwa kiwango cha changarawe katika hifadhi za Serengeti (1), Nyerere (3), Tarangire (1), Mkomazi (2), Saadani (1), Mikumi (1) na Ruaha (2).

Aidha, viwanja vya kutua helikopta (helipads)
vitano katika Mlima Kilimanjaro vilijengwa kwa kiwango cha zege kwa kuzingatia kanuni za TCAA na ICAO.

Sambamba na kununua mitambo 59 ya aina mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Dunia (Mradi wa REGROW) na IMF (Mradi wa TCRP).

"Mitambo iliyonunuliwa kupitia mradi wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (Resilient Natural Resources Management for Tourism and Growth - REGROW) ni motor grader 5, compactor 3, low loader 2,

"Malori 17, excavator 2, bulldozers 2, concrete mixers 5, matrekta 7, malori ya kubebea maji 5, magari ya sinema (cinema vans) 4,

"Yakiwemo magari ya kutolea elimu kwa wanafunzi na jamii “expedition trucks” 3 na malori ya kutengenezea magari (mobile workshop).Jumla ya shilingi 27,873,761,395.00 zilitumika kununua mitambo hiyo."

Amesema, mitambo iliyonunuliwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TCRP) ni motor grader 5.

Nyingine ni compactor 4, low loader 4, malori 15, excavator 4, magari madogo 7 (Landcruiser), concrete mixer 1, Back low loader 1 na malori ya kubebea maji 4) vyenye thamani ya shilingi 17,765,532,026 na zilitumika kununua mitambo hiyo.

"Mitambo hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya barabara katika Hifadhi zetu."

Ushirikishwaji

Ameema, katika kipindi cha miaka mitatu, shirika hilo limeendelea kuboresha mahusiano na jamii zilizo jirani na hifadhi za Taifa katika shughuli za uhifadhi na utalii.

"Kupitia mashirikiano haya zimepatikana faida mbalimbali ikiwemo kuibuliwa na Kutekelezwa kwa Miradi ya Kijamii “Support for Community Initiated Projects” (SCIPs)."

Amefafanua kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya miradi 59 ya kijamii yenye thamani ya shilingi 30,785,819,981 ilitekelezwa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 20,

Mabweni 2, nyumba 7 pacha za walimu, zahanati 12, nyumba pacha za wauguzi 6, miradi ya maji 6, barabara 5 zenye urefu wa kilomita 76 na bwalo la chakula kwa wanafunzi moja na ununuzi wa madawati 680.

"Miradi hii imetekelezwa katika Wilaya za Ruangwa, Makete, Mbeya, Mbarali, Mpanda - Halmashauri ya Nsimbo, Uvinza, Kigoma, Muleba, Bariadi, Bunda, Serengeti, Mbulu, Arumeru, Rombo, Longido, Mwanga, Same, Korogwe, Lushoto, Pangani,

Kilosa, Kilombero, Kilolo, Lindi na Ngorongoro (tarafa za Loliondo na Sale). Ujenzi wa miradi hii umesaidia kupunguza kero kwa jamii na kuongeza usalama wa wanafunzi.

"Na kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya sambamba na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

"Aidha, miradi hii imesaidia kuimarisha mahusiano mazuri kati ya jamii na hifadhi na kuifanya jamii kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa maliasili."

Vilevile akizungumzia kuhusu utekelezwaji wa Miradi ya Uzalishaji Mali (TANAPA Income Generating Projects-TIGPs) Kamishna Kuji amesema,jumla ya vikundi 138 vimewezeshwa miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, uchakataji wa viungo vya chakula na ufugaji.

"Jumla ya shilingi biliion 2.4 zilitumika kuwezesha miradi ya uzalishaji mali. Pia, Benki za Kijamii za Uhifadhi “Community Conservation Bank” (COCOBA) 159 zilianzishwa kupitia mradi wa REGROW na kupewa fedha mbegu kiasi cha shilingi 1,453,272,934."

Amesema, miradi hii imesaidia kuongeza wastani wa pato la wananchi katika maeneo husika na kupunguza utegemezi wa maliasili.

"Jumla ya wanafunzi 1,051 kutoka vijiji 60 vinavyotekeleza mradi wa REGROW wamepatiwa ufadhili wa masomo wenye thamani ya shilingi 4,273,315,700 katika vyuo mbalimbali vya kitaaluma hapa nchini.

"Ufadhili huu utasaidia kuongeza kiwango cha uelewa kwenye jamii na kuongeza uwezo wa uzalishaji mali kwenye jamii husika."

Pia, amesema TANAPA kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) na Shirika lisilo la kiserikali la “Frankfurt Zoological Society - FZS” imeendelea kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 57 vya wilaya za Serengeti,

Zikiwemo Morogoro, Kisarawe, Ulanga, Tunduru na Liwale na kutoa hati za kimila 16,243.

Amesema, kati ya hati hizo, hati 9,874 zilitolewa kwa jamii kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Nyerere na hati 6,612 zilitolewa kwa jamii kutoka kwenye vijiji vilivyo katika wilaya ya Serengeti vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

"Hata hivyo, tunaendelea kuandaa hati za kimila kwenye Wilaya za Bunda, Bariadi, Tarime, Meatu, Itilima na Busega.

"Uandaaji huu wa matumizi bora ya ardhi unasaidia kupunguza migogoro ya kimatumizi kati ya binadamu na wanyamapori kwenye maeneo husika na kuwajengea usalama katika umiliki wa ardhi kwa jamii zinazopakana na hifadhi."

Elimu

Amesema,kumekuwepo na ongezeko la idadi ya wananchi wanaofikiwa na elimu ya uhifadhi kutoka wananchi 169,245 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia wananchi 211,986 katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Desemba 2023 wananchi 125,389 wamefikiwa na elimu ya uhifadhi.

"Ongezeko hili linatoa uhakika wa kuwa na wanajamii wanaoelewa masuala ya uhifadhi na hivyo kuongeza uhakika wa ushiriki wa wananchi kwenye uhifadhi na ulinzi wa maliasili."

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Kamishna Kuji amesema,shirika limefungua vitalu na kugawa miche ya miti ya matunda, mbao na vivuli kwa wananchi.

Amesema, jumla ya miche 209,690 imegawiwa kwa wananchi katika kipindi husika katika hifadhi za Kilimanjaro, Milima ya Udzungwa, Arusha, Serengeti na Burigi-Chato.

Wakati huo huo, Kamishna huyo amesema Serikali imekamilisha utatuzi wa migogoro minne iliyodumu kwa muda mrefu kati ya vijiji na Hifadhi za Taifa Serengeti (vijiji 7 wilaya ya Serengeti),

Arusha (Farm 40/41 - Wilaya ya Arumeru), Tarangire (Kimotorok - Wilaya ya Simanjiro) na Manyara (Buger - Wilaya ya Karatu).

Pia, Serikali inaendelea kutatua migogoro na kufanya uthamini katika Hifadhi za Taifa za Ruaha (Ihefu), Milima ya Mahale (Vitongoji vya Kabukuyungu na Mahasa Kijiji cha Kalilani),

Saadani (Kitongoji cha Uvinje), Mkomazi (Kitongoji cha Kimuni), Arusha (Kijiji cha Nasula) na Kitulo (Wilaya ya Rungwe).

"Jumla ya vigingi 905 vimejengwa katika Hifadhi za Taifa za Serengeti (184), Ruaha (671), Ziwa Manyara (18) na Tarangire (32) pamoja na kulima MKUZA wenye urefu wa kilometa 609 (Tarangire - 242, Ruaha - 344 na Mikumi - 23) kufuatia utatuzi wa migogoro iliyokuwepo."

Amesema,Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi wa vijiji vya Nyatwali, Serengeti na Tamau ili kutwaa eneo la Ghuba ya Speke kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

"Na shirika limeendelea kukabiliana na kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu. Katika kipindi hiki, Shirika limeshughulikia kwa wakati matukio 4,954 yaliyoripotiwa.

"Pia, shirika limeweza kufunga visimbuzi (Global Positioning System - GPS collar) kwa makundi 12 ya tembo, makundi 12 ya simba na makundi 5 ya mbwa mwitu katika hifadhi za Mkomazi, Serengeti, Mikumi, Nyerere na Ruaha.

"Ufungaji huu wa visimbuzi kwa makundi hayo ya wanyama unasaidia ufuatiliaji wa karibu kwa makundi husika na kuweza kutambua mienendo yao ili kurahisisha udhibiti wanapotoka nje ya maeneo ya hifadhi."

Vilevile, kupitia mradi wa REGROW, Shirika limewezesha mafunzo kwa askari wa vijiji (Village Game Scout – VGS) 354 kutoka vijiji 39 ili kuwezesha kukabili kwa wakati matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Aidha, Shirika linaendelea na ujenzi wa vituo 8 vya Askari Uhifadhi katika maeneo ya kimkakati yaliyopo katika vijiji vinavyoathirika zaidi katika wilaya za Mbarali, Kalambo, Kilwa, Namtumbo, Ruangwa, Serengeti, Bunda na Bariadi. Vituo hivi vitasaidia askari kudhibiti kwa wakati wanyamapori wakali na waharibifu.

Kamishna Kuji ameongeza kuwa,shirika limeendelea kujikita katika matumizi ya teknolojia mbalimbali ambayo yamesaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news