Kamati ya Bunge yapitisha makadirio ya bajeti ya mwaka 2024/25 kwa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais,Utumishi na Utawala Bora

NA LUSUNGU HELELA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent Laurent Kyombo akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe wa Kamati kujadili na kuridhia bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati hiyo na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Amesema,baada ya majadiliano mazuri na maelezo ya ziada kutolewa kuhusiana na bajeti iliyotengwa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imeridhia.
“Tunawatakia matumizi mema ya fedha hizi pale zitakapokubaliwa kupitishwa katika vikao vya Bunge la Bajeti na tunahitaji kuona bajeti ya fedha hizi inaakisi matarajio ya msingi ya nchi yetu,” amebainisha Mhe. Kyombo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru Kamati hiyo kwa ushauri na kupitia bajeti hiyo kifungu kwa kifungu na kutoa maelekezo ya kuboresha kabla ya kuiwasilisha kwenye vikao vya Bunge la Bajeti.
“Mimi pamoja na timu yangu, tunatoa shukrani za dhati kwa jinsi mnavyotoa michango yenu yenye muelekeo wa kuboresha Utumishi wa Umma nchini ili kukidhi matakwa na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan” amesema Mhe. Simbachawene.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news