Waziri Mkuu awataka maafisa sheria na mawakili wa Serikali kuzingatia weledi

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali nchini kutekeleza majukumu kwa kuzingatia weledi, usawa na uadilifu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki bila kujali hali zao za kiuchumi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali wa Tanzania Mkutano ulifanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma tarehe 21 Machi, 2024. Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Upatikanaji wa Huduma za Kisheria kwa Wananchi ni Nguzo Muhimu kwa Ustawi wa Jamii."Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi, Machi 21, 2024 wakati akifugua mkutano wa Mkuu wa Chama cha Mawakili wa serikali Tanzania, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi wote, imeendelea kuchukua hatua kadhaa zikiwemo ujenzi wa miundombinu, uendelezaji wa rasilimali watu, maboresho ya mifumo na sheria mahsusi.

“Hatua hizo zimeendelea kutekelezwa sambamba na kuhakikisha uwepo wa watoa huduma hizo ili ziweze kupatikana pia katika maeneo ya vijijini kwa wananchi walio wengi,”amesema.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetekeleza mpango wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma, Vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki, Mahakama za Wilaya 27 pamoja na mahakama za mwanzo 14.

Ameeleza serikali inaendelea na ujenzi wa vituo jumuishi sita vya Geita, Simiyu, Njombe, Katavi, Songea na Songwe.

“Nampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuimarisha na kuboresha mifumo yetu ya utoaji haki nchini. “Jitihada mbalimbali anazozifanya zinatokana utashi wake katika kuhakikisha misingi ya demokrasia na utawala bora inaimarishwa na kuzingatiwa,”ameeleza.

Amesema Rais Dkt. Samia ameendelea kuhakikisha huduma za kisheria zinawafuata wananchi pale walipo kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuongeza na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za sheria.

Majaliwa amesema kutokana na maono na msukumo wa Rais Dk. Samia katika kipindi cha miaka mitatu kwenye tasnia ya sheria na utoaji wa haki,Serikali imewezesha Wananchi 415,280 na mahabusu 7,166 kufikiwa na huduma za kisheria bila gharama kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoka Mitaa/Vijiji 1,348 kwenye mikoa sita nchini.

“Huduma ya msaada wa kisheria inayoendelea kutolewa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufahamu wa wananchi kuhusu masuala ya kisheria na kusaidia utatuzi wa migogoro na utoaji wa huduma za kisheria katika masuala mbalimbali,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dk. Pindi Chana amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Samia Tanzania imekuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya Kimataifa.

Alisema,sababu ya Tanzania kuchaguliwa ni kutokana na uongozi bora chini ya Rais Dk.Samia.

Naye, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Juma ameeleza kuwa wataendelea kusimamia na kuhakikisha sheria zinatumika vyema katika utoaji wa haki kwa wananchi na kuyafikia malengo yaliyotajwa katika dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

“Kazi zetu zinaongozwa na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, hivyo tufanye kazi kwa kuzingatia hayo ikiwemo kujenga amani, mshikamano, kuboresha Maisha ya Mtanzania kwa kuelekeza nguvu ya sheria katika kuboresha Maisha yao na kuimarisha Utawala bora.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news