IAG kuongeza usimamizi wa mapato na matumizi

NA PETER HAULE

MKAGUZI Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai amesema ofisi yake itafanya mabadiliko makubwa katika taratibu za ukaguzi katika maeneo ya mapato na matumizi kutokana na mafunzo muhimu waliyoyapata katika Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA).
Wakaguzi wa Ndani katika nchi 27 Afrika wakiwa katika Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) ulioangazia taratibu za ukaguzi wa ndani, utawala bora na mazingira, uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha).

Hayo aliyasema jijini Arusha wakati wa kuhitimisha siku tano za Mkutano wa 10 wa Shirikisho hilo uliowakutanisha zaidi ya wajumbe 1200 kutoka nchi 27 za Afrika na nje ya Afrika.

Bw. Magai alisema kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia nchi yetu inatumia mifumo ya kielektroniki katika matumizi na ukusanyaji wa mapato, hivyo katika eneo hilo kumekuwa na vihatarishi vya udukuzi, kama nchi inatakiwa kujipanga vizuri kupitia wakaguzi wake.

“Tumejifunza mambo mengi katika mkutano huu, kuna baadhi ya maeneo inawezekana yalikuwa hayatekelezwi kwa ufanisi, kwa sasa tunakwenda kuongeza tija zaidi kwa kuwa wakaguzi wetu sasa wanaweza kufanya kaguzi za kitaalamu zaidi kuliko ilivyokuwa awali,” alisema Bw. Kigai.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai (kushoto) na Msaidizi wake, Bw. Mwanyika Semroki, wakifuatilia mada za ukaguzi wa mazingira siku ya mwisho ya Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Bw. Magai amesema kuwa Mkutano huo wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika uliofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, umechochea hamasa ya kufanyakazi kwa weledi mkubwa unaoambatana na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha taratibu muhimu katika eneo la ukusanyaji mapato, matumizi na pia mazingira na uatawala bora zinafuatwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Wizara ya Fedha, Bw. Lisius Mwenda, (wa kwanza kulia), akifuatilia mada za kikaguzi kuhusu utawala bora wakati wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Akizungumzia kuhusu ukaguzi wa mazingira, Bw. Kigai alisema kuwa ni eneo jipya ambalo wakaguzi waliona sio muhimu lakini kwa sasa limepewa uzito mkubwa ukizingatia kwa sasa kuna athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mafuriko, joto na maporomoko ya ardhi jambo ambalo mkaguzi anatakiwa kuwa na jukumu muhimu katika kuhakikisha taasisi zote za umma zinajipanga katika kukabiliana na na masuala hayo.

Aidha alisema kuwa mkutano huo ulijumuisha eneo la Utawala bora na masuala ya kitaalamu katika eneo la ukaguzi ambao ulifanyika kwa siku mbili na kufuatiwa na Kongamano lilochukua siku tatu ambalo lilijikita katika masuala ya ukaguzi wa ndani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, akitoa mafunzo ya Afya yanayomwezesha mkaguzi wa ndani kufanya kazi zake kwa ufanisi, wakati wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Alisema lengo kubwa lilikuwa kuwakutanisha wakaguzi wa ndani wa Afrika na nje ya Afrika kwa ajili ya kupata uzoefu kutoka nchi mbalimbali katika maeneo kadhaa yakiwemo ya ukaguzi wa hesabu, vihatarishi na mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news