Wanahabari nchini wapewa darasa kuhusu Riba ya Benki Kuu (CBR)

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI wa Utafiti na Sera za Uchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango amesema kuwa,Riba ya Benki Kuu (CBR) hutolewa kama riba elekezi kwa mabenki kuweza kukopa fedha kutoka Benki Kuu nchini.
Dkt.Missango ameyabainisha hayo leo Aprili 8,2024 baada ya BoT kukutana na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam ili kutoa elimu kuhusiana na mfumo mpya wa Sera ya Fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu (CBR).

Sambamba na uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha kupandisha riba hiyo kutoka asilimia 5.5 hadi 6 ambapo itatumika kwa robo ya pili kuanzia Aprili hadi Juni,mwaka huu.

Elimu hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Aprili 4,mwaka huu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba kueleza kuwa, uamuzi wa kupandisha riba umetokana na maoteo au uchambuzi uliofanyika Machi,2024.

Uchambuzi ambao ulionesha kwamba endapo kiwango cha riba kingebakia asilimia 5.5, kulikuwa na viashiria vya mfumuko wa bei kuongezeka.

Dkt.Missango amefafanua kuwa, “Ni riba ambayo BoT inatoa kama riba elekezi kwa mabenki kuweza kukopa fedha Benki Kuu ili ziweze kufanyia shughuli zao, ikiwemo kukopesha."

Mbali na hayo amesema, riba hiyo hutumika pia kudhibiti mfumuko wa bei kwa kudhibiti kiwango cha fedha kilichopo kwenye mzunguko nchini.

“Benki Kuu ikiona kiwango cha fedha kilichopo katika uchumi kinaelekea kuwa zaidi ya pale kinapotakiwa, hutumia mfumo huu ili kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza ukwasi kwenye mzunguko."

Amesema, mfumo wa sera ya fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu unasaidia mabenki na taasisi nyingine za fedha kupanga viwango vyao vya riba na sio kuweka ukomo wa riba kwa mabenki na taasisi zinazotoa mikopo.

“Kwa sababu hii ni riba elekezi, inasaidia mabenki na taasisi nyingine za fedha kuweza kupanga viwango vyao vya riba.

"Mwanzoni wakati tunaanza kutumia mfumo huu watu walifikiri kuwa Benki Kuu inaenda kuweka ukomo wa riba, si kweli,”amesisitiza Dkt.Missango.

Akizungumzia namna ya kuipata Riba ya Benki Buu,, Dkt.Missango amesema, kuna vigezo vingi ambavyo huwa vinatumika.

"Tunazingatia mwenendo wa uchumi hapa nchini na mwenendo wa uchumi duniani. Duniani kwa sababu sisi Tanzania pia tunaagiza bidhaa na tunauza bidhaa nchi za nje.

"Kwa hiyo, hayo ndiyo makundi mawili, uchumi wa hapa nchini tunaangalia viashiria vingi vya uchumi ikiwemo mfumuko wa bei, ukuaji wa uchumi, umuhimu wa kuhakikisha kwamba tunaendelea kuweka mazingira sahihi ya kuongeza mauzo yetu nchi za nje pamoja na vitu vingine.

"Kwa hiyo, hii riba tunapoiona ya asilimia 6 ina vitu vingi sana, na hiyo itakuwa imeangalia mwelekeo, imechukua yale ambayo yameshatokea, sasa hivi tulipo, tunakoelekea ndipo mnakuja na hiyo riba ambayo mmeamua kama Benki Kuu.

"Kwamba sasa, tunafikiri kwamba kwa jinsi ambavyo mwelekeo wa kiuchumi unavyoashiria basi tunatakiwa kuwa na riba ya kiasi gani.

"Lengo kuu la kuweka riba hii ya Benki Kuu ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na mfumuko wa bei ambao unalingana na malengo tuliyojiwekea, na vile vile kuhakikisha kwamba tunaendelea kusaidia ukuaji wa uchumi.

"Mfumuko wa bei ukiwa mdogo unasaidia vile vile kuimarisha urari wa biashara nchi za nje.

"Kwa sababu leo hii hapa kama mfumuko wa bei ukiwa mkubwa ina maana kwamba hata uwekezaji hapa nchini utapungua, vipato vya watu pia vitapungua."

Dkt.Missango amefafanua kuwa,mfumuko wa bei unasaidia uwezo wa mtu mmoja mmoja kununua bidhaa na huduma.

"Kwa hiyo ndiyo sababu tunahakikisha mfumuko wa bei unaendelea kuwa mdogo ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira ya wazalishaji, waweze kuzalisha zaidi na bidhaa zingine zitauzwa hapa nchini na zingine zitauzwa nje ya nchi.

"Kama mtu atazalisha, ataweza kuuza hapa nchini, ina maana na yeye atakuwa amepunguza, kama tuna bidhaa nyingi zinazouzwa hapa nchini ina maana tutapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

"Na utakapopunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje tayari unakuwa umeimarisha sekta yetu ya nje.

"Kwa hiyo ikiwa kama umeongeza uzalishaji kila mara umeongeza uzalishaji, mfumuko wa bei ni mdogo, viwanda vinazalisha, watu wanazalisha, wanalima ina maana kwamba baada ya muda ule urari utaimarika zaidi badala ya kupungua.

"Ndiyo umuhimu wa ile riba kuweza kudhibiti mfumuko wa bei, kuna faida nyingi ikiwemo kuimarisha urari wa biashara kati ya Tanzania na nchi zingine."

Vile vile akifafanua kuhusu mwelekeo wa urari, Dkt.Missango amesema, wanatarajia kuendelea kuimarika na nakisi kuendelea kupungua.

"Moja, kwa sababu hata uchumi wa Dunia unazidi kuimarika ukilinganisha na kule tulikotoka.

"Kwa hiyo taarifa nyingi ambazo tumezipata kwa mfano kwenye hiyo ripoti ya robo ya kwanza tumeona uchambuzi uliofanyika unaonesha kabisa kwamba mfumuko wa bei katika nchi nyingi utaendelea kupungua.

"Ukiendelea kupungua ina maana kwamba sisi tunapoendelea kuagiza bidhaa kutoka nje kama tulikuwa tunaagia kwa dola 10 ina maana kwamba tunapoagiza tena katika kipindi kijacho hakutakuwa na ongezeko kubwa kuliko awali.

"Kwa hiyo tutakuwa tunapata unafuu, lakini tumeona kwamba nchi nyingi uchumi unaendelea kuimarika, ukiendelea kuimarika huko ina maana kwamba sisi tutakapokuwa tunauza bidhaa zetu nchi za nje, watu wana kipato cha kutosha cha kuweza kununua bidhaa zetu.

"Lakini, vile vile tumeona bei ya mafuta na bidhaa zingine tunatarajia kwamba itaendelea kuwa tulivu, kwa hiyo kwa upande wote huo wa uchumi wa dunia ina maana kwamba tunatarajia kupata nafuu zaidi.

"Lakini, kwa uchumi wetu hapa nchini tunatarajia vile vile kuendelea kuimarika, zile changamoto tulizokuwa nazo zinaendekea kupungua.

"Kwa hiyo mwelekeo, hivi vitu vyote ukiviweka kwa pamoja vinaashiria kwamba mwelekeo wa urari wa biashara nchi za nje tunatarajia kuendelea kuimarika na vile vile utachagizwa na Sekta ya Utalii,"amefafanua Dkt.Missango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news