Dkt.Yonazi awashukuru Jukwaa la Viongozi Tanzania kwa msaada wa shilingi milioni 13.7 kwa waathirika Hanang

DODOMA-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amepokea msaada wa shilingi milioni 13.7 kutoka kwa wanachama wa kundi sogozi (WhatsApp) liitwalo Viongozi Tanzania.

Akipokea msaada huo katika hafla hiyo iliyofanyika jana ofisini kwake Mei 6,2024 mjini Dodoma,Dkt.Yonazi amewashukuru wanachama wa kundi hilo.

Ni kwa kujitoa kwao kwenda kwa waathirika hao wa maporomoko ya udongo, tope, mawe na magogo kutoka mlima Hanang' mkoani Manyara yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2023.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera Bunge na Uratibu,Dkt Jim Yinazi(kushoto) akipokea msaada wa shilingi milioni 13.7 kutoka kwa Mratibu Mkuu wa Kundi la Viongozi Tanzania Benjamin Thompson(kulia) kwa ajili ya waathirika wa mafuriko ya Hanang',huku mmoja wa Wanachama wa kundi hilo Mhandisi Archard Kato (katikati) akishuhudia.

Dkt.Yonazi amesema,msaada huo,pamoja na misaada ya wasamaria wengine inaunga mkono jitihada za serikali zinazoendelelea katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika hao ikiwemo kujengea nyumba 108, ili wanaendelee kujitafutia riziki na kujiletea maendeleo yao.

Aidha, Dkt. Yonazi ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa na desturi ya kuwakimbilia wahitaji pale ambapo wanapata athari za majanga mbalimbali.

"Tunawashukuru wenzetu wa kundi la Viongozi Tanzania kwa uzalendo waliouonesha kwa ajili ya mchango huu mkubwa walioutoa, niwaombe Watanzania wenzangu tuzidi kushikana mkono hasa nyakati hizi ambapo sehemu nyingi nchini yametokea majanga mbalimbali,hivyo ni jambo jema kuendelea kushirikiana kuwasaidia ndugu zetu, "alisema Dkt. Yonazi

Wajumbe wawili wa kundi hilo ambao ni Ndg.Benjamin Thompson, ambaye ndiye Mratibu Mkuu wa kundi hilo, pamoja na Mhandisi Archard Kato,ambaye ni mmoja wa Wanachama wa kundi hilo, waliwawakilisha wanachama wengine zaidi ya 600.

Ni walioko kwenye kundi hilo, ambao ni viongozi mbalimbali wa serikali,viongozi wa taasisi za umma,viongozi wa sekta binafsi,wahadhiri na viongozi wa vyuo vikuu,viongozi wa vyama vya siasa,viongozi wadiaspora n.k.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera Bunge na Uratibu,Dkt Jim Yinazi akifafanua jambo mara baada kupokea msaada 13.7m/- kwa ajili ya waathirika wa mafuriko ya Hanang kutoka kwa Jukwaa la Viongozi Tanzania.

Bw.Thompson alisema michango hiyo ilikusanywa kutoka kwa wanachama 145 tu kati ya wote walioko kwenye wa kundi hilo, ambao ndio waliweza kuchangia kwa wakati huo.

"Mkusanyaji wetu alikuwa ni Zamaradi Kawawa,ambaye alifanya kazi nzuri sana na kwa uaminifu mkubwa.Baada ya kumaliza kazi hiyo.

"Tulikubaliana kwamba aweke pesa hizo kwenye akaunti ya maafa iliyopo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu,na aliweka pesa hizo Desema 27,2023.Sasa hili lililofanyika hapa leo lilikuwa ni kukabidhi tu karatasi ya malipo yaani pay in slip,"alisema Bw. Thompson.

Naye Mhandisi Kato, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya kutengeneza mvinyo ya Alko Vintages iliyopo Dodoma, alisema wanachama wa kundi hilo wameguswa na janga hilo la Hanang na hivyo kuona umuhimu wa kutoa michango hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na majanga kama hayo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera Bunge na Uratibu,Dkt Jim Yinazi(wa tatu kushoto) akitoa mkono wa shukrani kwa Mratibu Mkuu wa Kundi la Viongozi Tanzania Benjamin Thompson(wa tatu kulia) mara baada ya makabidhiano ya 13.7m/- kwa ajili ya waathirika wa mafuriko ya Hanang.Wengine pichani ni Naibu Katibu Mkuu ofisi hiyo Bw. Anderson Mutatebwa (wa pili kutoka kushoto),Mhasibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Anthony Chayeka (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Brig Jen Hosea Ndagala (wa pili kulia) pamoja na mmoja wa Wanachama wa kundi hilo Mhandisi Archard Kato(kushoto).

"Tunakuahidi kwamba tutaendelea kuisaidia serikali kwa kidogo tulicho nacho katika kukabiliana na athari za majanga kama haya,na tungependa kuona hili jambo linaenea kwa watanzania wengi,yaani hata kabla ofisi yako haijafika au serikali haijafika.

"Angalau watanzania wenyewe wawe wanafanya jambo la mwanzo kwa uzalendo wao katika kukabiliana na mambo hayo hasa ya dharula ambayo hakuna mtu ambaye amepanga yatokee hasa hasa mafuriko,"alisema Mhandisi Kato.

Janga la Hanang' lilitokea Desemba 3, mwaka jana mkoani Manyara na kusababisha vifo ya watu zaidi ya 80, huku mamia wengine wakiachwa bila makazi, uharibifu mkubwa wa miundombinu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news