DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea timu ya wataalamu kutoka Ofisi za Umoja wa Afrika (AUC) wanaoratibu utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za hali ya hewa wa Intra-ACP Climate Services and related Applications Programme (ClimSA).

Timu hiyo ya wataalamu walitembelea Ofisi Kuu ya Utabiri wa Hali ya Hewa iliyopo Ubungo Plaza, Dar es salaam kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa mitambo ya ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa na utabiri wa hali ya hewa, inayoitwa PUMA STATION iliyotolewa kwa TMA kupitia mradi wa ClimSA.
Mradi wa ClimSA unatekelezwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AUC), ikiwemo Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (European Union).
Mradi huu unalenga kuimarisha zaidi uwezo wa nchi wanachama wa AU katika kufuatilia mifumo ya hali ya hewa kupitia teknolojia ya satelaiti ili kuboresha zaidi utabiri wa hali ya hewa na huduma za hali ya hewa kwa ujumla.