DAR-Zaidi ya washiriki 1,200 kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam, Tanzania, kushiriki katika Mkutano wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF) utakaofanyika kuanzia Mei 29 hadi 31, 2025, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 22, 2025 Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba, alisema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujadili masuala nyeti yanayohusu maendeleo ya intaneti na teknolojia barani Afrika.“Mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu, kwa mujibu wa takwimu za ITU za mwaka 2024 ni asilimia 38 pekee ya Waafrika wanaotumia intaneti ya uhakika, huku kwa Dunia nzima ni asilimia 68. Hii inaonyesha pengo kubwa,"amesema Mhandisi Magomba.
Ameongeza kuwa, mkutano huo utatoa fursa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kujadiliana kuhusu njia za kuongeza upatikanaji wa intaneti kwa wote, kuondoa tofauti ya matumizi kati ya mijini na vijijini, pamoja na kuimarisha usalama wa mtandao.
Aidha, teknolojia ya Akili Unde (AI) itapewa kipaumbele, ikizingatiwa mchango wake mkubwa katika kurahisisha kazi na kuongeza ufanisi, hususan katika zama za Nne na Tano za Mapinduzi ya Viwanda.
“Tunahitaji kuangalia namna bora ya kutumia teknolojia hii kwa maendeleo ya Afrika,”amesema Mhandisi Magomba.
Mkutano huo pia utajadili mahusiano ya kimataifa katika usimamizi wa mtandao, kwa kuzingatia kuwa suala hilo linahitaji ushirikiano wa mataifa yote na si la nchi moja pekee.









