KIGOMA-Juni 19, 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma limefunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi Na.ECO 9652/2025.
Ni dhidi ya washtakiwa Bw. Onesmo Janks Nimbuga (34) ambaye ni Muuguzi Mkunga katika Kituo cha Afya Mtendeli pamoja na Bi. Annie Newton Mabago (37) aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho.
Wote, wametiwa hatiani kwa makosa 22 ya matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri,ubadhirifu na ufujaji, kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329.
Makosa mengine ni Kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 vya Kanuni za Adhabu Sura ya 16, marejeo ya 2022.
Kwamba, washtakiwa hao wakiwa katika Kituo cha Afya Mtendeli walifanya malipo hewa kwa kuandaa hati ya malipo na kughushi kuonesha kuwa walinunua betri ya sola N200 yenye thamani ya shilingi 586, 200 na badala yake walitumia kiasi hicho cha fedha kwa matumizi yao binafsi.
Washtakiwa wamehukumiwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi milioni 1,000,000.
Shauri hili lilikuwa likisikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko Mh. Ambilike Japhet Kyamba na kuendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka TAKUKURU (M) Kigoma Bw. Jackson George Lyimo.
