Profesa Shemdoe aelekeza magari 14 ya usimamizi wa miradi ya TACTIC kufanya kazi iliyokusudiwa

DAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaelekeza Mameneja na waratibu wa Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kuhakikisha magari 14 aliyoyakabidhi yanakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa ya usimamizi wa mradi huo ili wananchi wanufaike na barabara, masoko na stendi zinazojengwa kupitia mradi huo.
Prof. Shemdoe ametoa maelelezo hayo leo Februari 21, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo kwa Mameneja wa TARURA wa Miji 12 ya kundi la kwanza la Mradi wa TACTIC, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Millenium Tower Kijitonyama, Dar es Salaam.

“Magari haya yamenunuliwa kwa fedha za umma, hivyo yatunzwe na yakatumike kwa kazi za usimamizi wa mradi wa TACTIC na si nyinginezo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewata wakandarasi walio kwenye maeneo ya utekelezaji wa miradi ya TACTIC, kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia mikataba waliosaini ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, na kuongeza kuwa Serikali haitosita kusitisha mikataba inayosuasua kwa mujibu wa sheria na vipengele vya mikataba husika.

Prof. Shemdoe amesema Serikali haina changamoto ya kukosa fedha za utekelezaji miradi, kwani pindi mkandarasi akiwasilisha hati ya maombi ya malipo analipwa kwa wakati, hivyo hakuna sababu ya wakandarasi kushindwa kukamilisha na kukabidhi miradi kwa wakati.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Albert Kyando ameishukuru Serikali kwa kuwakabidhi magari yatakayowawezesha kusimamia miradi ya TACTIC kwa karibu na kuahidi kuwa watayatunza kama Prof. Shemdoe alivyoelekeza kwa maslahi ya umma na taifa.
Naye, mmoja wa madereva waliokabidhiwa magari hayo kutoka Jiji la Arusha Bw. Joshua Magati, amesema watayatunza magari hayo kama alivyoelekeza Prof. Shemdoe, na kuongeza kuwa watazingatia muda wa kuyafanyia ukaguzi na matengenezo pamoja na kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa ya usimamizi wa miradi ya TACTIC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here