Tume ya uchunguzi yaongezewa muda hadi Aprili 3,2026

DAR-Mamlaka ya Uteuzi imeongeza muda wa siku arobaini na mbili (42) kuanzia tarehe 20 Februari, 2026 Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ili Tume iweze kukamilisha uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025 na kuitaka ikamilishe kazi na kuwasilisha Taarifa yake kabla au ifikapo tarehe 3 Aprili, 2026. Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa katika gazeti la serikali Tume imeongezewa muda huo ili kutoa fursa na muda wa kutosha kwa kila mwenye taarifa, ushahidi au maoni, aliyepo nchini au nje ya nchi, kuwasiliana na Tume ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote, au taasisi yoyote, itakayokosa nafasi ya kusikilizwa.

Sababu nyingine za kuongeza muda ni pamoja na zifuatazo Wingi na mchanganyiko wa taarifa zilizokusanywa, na zinazoendelea kukusanywa, na Tume ambazo zinahitaji muda zaidi wa kufanyiwa uchambuzi wa kina, Tume kulazimika kutumia Wataalamu (experts) kutoka ndani na nje ya nchi wenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kisayansi, na uchambuzi wa kidijitali wa baadhi ya taarifa na vielelezo kutokana na aina ya matukio na ushahidi uliokusanywa hadi sasa, na unaoendelea kuwasilishwa.
Sababu nyingine ni Tume kubaini mapengo kadhaa katika taarifa na vielelezo vilivyokusanywa hadi sasa hivyo kuhitaji kutafuta au kupata taarifa zaidi ili kukamilisha ushahidi kwa kila hoja inayohusika, Kutoa fursa kwa wadau wachache muhimu ambao kwa sababu mbalimbali bado hawajafika mbele ya Tume, licha ya kupelekewa mialiko zaidi ya mara moja.

Taarifa hiyo imewataja wadau hao kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa dini, viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi na Wingi wa wananchi wengine wanaoendelea kufika mbele ya Tume kuwasilisha taarifa, ushahidi na ushauri wao.

Kutokana na fursa hiyo ya Tume kuongezewa muda Tume kupitia Mwenyekiti wake Jaji Othuman Chande inatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuwasilisha ushahidi kwenye Tume kwa kutumia njia zote zilizokuwa zimeainishwa awali ambazo ni majadiliano ya ana kwa ana, mawasilisho ya maandishi (written submissions) kwa njia ya posta au tovuti maalumu ya Tume; barua pepe; ujumbe mfupi wa simu (SMS); kujaza dodoso maalumu kwenye mtandao (www.tume.uchunguzi.go.tz), au kwa kupitia mitandao mingine ya kijamii.

Pia, tume hiyo imetoa wito maalumu kwa baadhi ya viongozi wa dini, viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi ambao wamepewa mialiko na Tume lakini bado hawajafika mbele ya Tume kutumia fursa hii kufika au kuwasiliana na Tume kutoa mchango wao katika uchunguzi unaoendelea kwa manufaa ya wananchi, wadau na nchi kwa ujumla.
Taarifa hiyo pia kupitia Gazeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaeleza Umma umuhimu wa kuendelea kuipa Tume ushirikiano ili kuiwezesha kukamilisha kazi yake ya uchunguzi.

Kama ilivyokuwa mwanzo, Tume itaendelea kufanya vikao vya wazi (public hearing) isipokuwa pale ambapo mashahidi kwa faida ya usalama wao hawapendi majina yao, sura na taarifa zao zitolewe kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Mpango Kazi, Tume ilipaswa kuwasilisha Taarifa kabla au ifikapo tarehe 20 Februari 2026 ikiwa ndani ya siku 90, ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 20 Novemba, 2025 mara baada ya kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here