DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) leo Februari 25, 2026, amekabidhi magari mapya 72 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha kuwafikia walipakodi, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Chuo cha Kodi, jijini Dar es Salaam, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, Serikali itaendelea kuiunga mkono TRA katika kukidhi mahitaji muhimu ya kiutendaji, ikiwemo magari hayo mapya yaliyogharimu shilingi bilioni 24.8.“Lengo kuu la Serikali ni kuongeza makusanyo na kuimarisha utendaji wa TRA, hivyo, nawasihi muyatumie magari haya kwa uangalifu na kuyatunza ili yaakisi madhumuni yaliyokusudiwa,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa walipakodi na kuhakikisha njia zote za mawasiliano na huduma zinaboreshwa ili kuwafikia wananchi kwa uharaka, uwazi na ufanisi zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Uledi Mussa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka hiyo katika kutelekeza majukumu yake, ikiwemo kuwaongezea watumishi hivi karibuni.
Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda, ameahidi kutumia magari hayo ambayo ni vitendea kazi muhimu ili kuimarisha utoaji huduma kwa walipa kodi.
Aliongeza kuwa,TRA itaongeza ushirikiano na wafanyabiashara ili kuendelza utulivu wa usimamizi wa kodi nchi nzima na kuyaishi matamanio ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa karibu na kuwahudumia ipasavyo walipakodi.








