NA DIRAMAKINI
MAMLA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeanza kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI) katika kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.
Akitoa ujumbe rasmi wa maadhimisho hayo leo Machi 23, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt.Ladislaus Benedict Chang’a amesema, kaulimbiu ya mwaka huu, “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama,” inalenga kuhimiza matumizi sahihi ya data za hali ya hewa katika kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo endelevu.Dkt. Chang’a ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) amesema, matumizi ya mifumo ya kidijitali kama Digital Meteorological Observatory (DMO) na mifumo ya utabiri yameongeza ufanisi katika ukusanyaji na uchambuzi wa data.
Amesema, teknolojia hiyo inasaidia kutoa taarifa sahihi kwa wakati na kuboresha mifumo ya maamuzi katika sekta mbalimbali.
"Katika juhudi za kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini, TMA haijabaki nyuma katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ikiwemo matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence-AI) ili kuboresha utoaji wa huduma na mifumo ya utoaji wa maamuzi katika sekta mbalimbali nyeti hususan zile zinazoathiriwa sana na hali ya hewa na umma kwa ujumla. "
Dkt.Chang’a amesema, katika kukabiliana na mabadiliko ya maendeleo ya kiteknolojia, wataalamu wa TMA wamebuni mifumo ambayo ni pamoja na Mfumo wa mawasiliano wa ubadilishanaji wa data na taarifa za hali ya hewa kutoka vituo vya hewa nchini na kuzikusanya kwenye kituo kikuu cha utabiri kilichopo Dar es Salaam.
Ni kabla ya kubadilishana na chi nyingine duniani ujulikanao kwa jina la “Digital Meteorological Observatory (DMO)”, pia mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa.
Pia, amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuboresha huduma zake kwa watumiaji wa bahari na maziwa kupitia mfumo wa “Marine Meteorological Information System (MMIS)” na “Meteorological Aviation Information System (MAIS)”.
"Mifumo hii imeimarisha uangazi, usimamizi wa data za hali ya hewa, usambazaji wa taarifa, na utoaji wa huduma."
Amesema, juhudi hizi ni utekelezaji wa dira ya TMA ya kuwa, “Kitovu bora cha huduma za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii”.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania