LINDI-Kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Askari Polisi Wanawake wa mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na askari wanawake kutoka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama wametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wafungwa na mahabusu katika Gereza Kuu la mkoa huo pamoja na wanafunzi wenye changamoto ya akili katika Shule ya Msingi Mpilipili.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Polisi Jamii mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Monica Sehere, alisema askari wanawake wamejitolea kwa hali na mali hadi kufanikisha malengo ya kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii na pia msaada huo utakuwafaraja kwao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Gereza la Mkoa wa Lindi, Mrakibu Mwandamizi wa Magareza SSP Devid Mkombya, alishukuru kwa msaada huo akisema unaleta faraja kubwa kwa wafungwa na mahabusu waliopo gerezani hapo na kuonyesha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuwa karibu na jamii hata kwa walio katika mazingira magumu.
Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Mpilipili, Mlopokade, alitoa shukrani kwa askari hao huku akitoa wito kwao kuwa mabalozi wa kuhamasisha wazazi wenye watoto wenye changamoto za akili kuwapeleka watoto hao shule ili waweze kupata elimu na huduma stahiki.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa inatarajiwa kufanyika Machi 8, 2026 katika Wilaya ya Ruangwa.












