Endeleeni kuishi viapo vyenu mkizingatia mila na desturi-Jaji Mkuu

NA HABIBA MBARUKU
Mahakama Dodoma

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewaapisha Mahakimu Wakazi wapya wawili, Mhe. Moonlight Martin Tupa na Mhe. Deus Philo Nyimbo na kuwataka Mahakimu hao kuviishi viapo vyao huku wakizingatia mila na desturi za maeneo wanayofanyia kazi.
Hakimu Mkazi Mpya, Mhe. Moonlight Martin Tupa (wa kwanza kulia) akila kiapo cha uadilifu mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele) tarehe 04 Machi, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Wanaoshuhudia wa pili kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert.

Mhe. Masaju ameyasema hayo Machi 4, 2026 mara baada ya zoezi la uapisho wa Mahakimu hao lililofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kiapo au viapo, na kuna viongozi wanatajwa moja kwa moja kwamba wao kabla ya kuanza majukumu yao watalazimika kula kiapo na moja ya wanaotajwa katika Katiba hiyo ni Majaji na Mahakimu, tuliokwisha kula kiapo maneno haya ya kiapo tunayafahamu, wasiwasi wangu ni kwamba kama tunayatilia maanani,” amesema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza Mahakimu hao kuendeleza tamaduni za maeneo husika.

Akizungumzia kuhusu uadilifu, Mhe. Masaju amesema kuwa, uadilifu unaanzia kwenye kiapo ambacho wametumia kuapa hivyo ni vema wakakiheshimu na kukitekeleza kwa uadilifu ili wasiwe wamelitaja bure Jina la Mwenyezi Mungu na kuwa heshima haitokani na cheo bali heshima inatokana na huduma.

“Uadilifu unaanzia kwenye kiapo, juzi nilipoongea na wenzenu niliwaambia tusimchukulie Mungu poa, Mungu mwenyewe anatamka, anaelekeza kwamba jina lake lisitamkwe bure. Kwenye hicho kiapo mlipokuwa mnamaliza mmesema Eee Mwenyezi Mungu nisaidie, uadilifu wenu unaanzia hapa kwenye kiapo kile,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Ameongeza kwamba, Mahakama ina kiapo ambacho ikiwa watakikiuka watawajibishwa wasipozingatia kiapo hicho Mungu atawaadhibu mwenyewe hapa duniani au baada ya kufa ikiwa hawatatubu.
Mahakimu Wakazi wapya walioapishwa wakisaini viapo vya uadilifu mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya uapisho iliyofanyika tarehe 04 Machi, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Kwa kawaida kiapo kina adhabu na sisi hapa tuna adhabu mbili, moja ukikiuka hicho kiapo unaweza kushtakiwa kwa kosa la jinai ukawajibishwa, cha pili unawajibishwa na Mwenyezi Mungu ambaye umeapa kwake na ndiye unayemuomba akusaidie, na yeye ana namna nyingi ya kuwawajibisha, anaweza akakusubiri wakati umeshakufa kama hukutubu akakuwajibisha huko huko, lakini mara nyingi huwa naona wala rushwa na wale wanaokiuka maadili anawawajibisha hapa hapa duniani kwanza, watambue wajibu wao wamrudie Mwenyezi Mungu,” amesema Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa, kila anayehitaji kuheshimiwa anapaswa kuheshimika pia kutambua kuwa jamii itamheshimu kwa namna anavyotenda na si kwa nguo anazovaa na cheo alichonacho, akiongeza kuwa hawahitaji kujitutumua bali wawe wanyenyekevu na kuwaheshimu watu wengine katika sehemu zao za kazi na jamii yote kwa ujumla.

Akizungumza kuhusu kutambua mila na desturi za jamii za Kitanzania, Mhe. Masaju amesema kwamba, kila Hakimu anapaswa kuzingatia na kuziheshimu mila na desturi kama ambavyo Katiba inazitambua na kuziheshimu Katiba za Kiislamu, akisisitiza kuwa Mahakama za mwanzo zinalazimika kukaa na washauri wa Mahakama kwenye mashauri yanayohisha sheria za kimila au Kiislamu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisaini viapo vya Mahakimu Wakazi aliowaapisha tarehe 04 Machi, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Katiba inatambua hizi mila na desturi za Tanzania, inatambua viapo, sisi tutatakiwa kufuata mila na desturi, na ndio maana tuna Mahakama hapa zinatambua hizi mila na desturi, na Mahakama za Mwanzo mnapokuwa mnatekeleza majukumu yenu katika yale mashauri yasiyokuwa ya jinai, ni pamoja na kuzingatia hizo mila, desturi na sheria za Kiislamu,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, si lazima mtu kufanya kazi katika sehemu aliyozaliwa na kwamba wapo watakaoenda kufanya kazi mijini au vijijini hivyo ni lazima wazitambue mila na desturi za mahali husika, ili waweze kutatua kwa haki migogoro mbalimbali inayohusu mila na desturi au migogoro katika ndoa za kiislamu kulingana na mila na desturi husika.

Aidha Jaji Mkuu ameeleza kwamba, katika kutatua migogoro hiyo pale watakapoona inafaa, watapaswa kukaa na washauri wa Mahakama ambao watawashauri kwa hekima katika kuzingatia mila na desturi katika kutoa hukumu huku akishauri Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kujumuisha masuala ya mila na desturi ili zitambulike na kurahisisha wakati wa utoaji hukumu.

Ametaja uhumimu wa Washauri wa Mahakama kuwa ni pamoja na kutoa ushauri ili kutoa hukumu ya haki kwa kuzingatia jamii, kusaidia kutatua migogoro ya kijamii ya kiislamu katika masuala ya ndoa pamoja na kutoa ushauri wa kimila kulingana na mazingira, pia kuwashirikisha katika maamuzi pale Mahakama itakapoona kwa maslahi ya haki inalazimu kufanya huvyo, au pale Mahakama itakapoombwa na mmoja wapo wa wadaawa katika shauri husika.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Mahakimu Wakazi wapya wawili aliowaapisha leo tarehe 04 Machi, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Katika hafla hiyo pia walikuwepo Mahakama Wakazi wapya 90 wanaoendelea na Mafunzo elekezi baada ya kuapishwa hivi karibuni.

Amesema kuwa ikiwa Wazee wa mila na Machifu watatungiwa sheria ya kuwatambua, pamoja na wajibu mwingine, wajibu wao utakuwa ni ule ulioelezwa katika Ibara ya 19(3) na Ibara ya 30(2)(a) akiyataja majukumu hayo kuwa ni usalama wa jamii, amani katika jamii na umoja wa kitaifa, kadhalika watasaidia katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa, ulinzi na utunzaji wa mazingira, huku akitilia mkazo kuwa watu hao ni muhimu katika utatuzi wa migogoro kwa sababu jamii inayowazunguka inawasikiliza na kuwaheshimu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju ameeleza majukumu ya Serikali za Mitaa ambazo zina wajibu wa kuhimiza utawala wa sheria katika jamii, amani katika jamii na umoja wa kitaifa huku akieleza kuwa, Serikali za Mitaa pia zinapaswa kutekeleza shughuli zake ipasavyo kwa kutumia demokrasia, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi akirejea Ibara ya 146(1) pamoja na Ibara ya 146(2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaeleza wazi madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa.

Kadhalika, Jaji Mkuu amesema kuwa, mategemeo ya Mahakama ni ya kwanza kutii kiapo kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza juu ya kuishi viapo sambamba na kuziheshimu mila na desturi za Tanzania, huku akiwakumbusha pia kuzingatia mila katika mavazi kwa wanawake kujistiri kwa heshima na wanaume kuvaa mavazi yenye hadhi na heshima.
Mahakimu Wakazi wapya waliokuwa wakiendelea na mafunzo elekezi pamoja na walioapishwa wakisikiliza kwa makini hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju baada ya zoezi la kuwaapisha Mahakimu wapya wawili tarehe 04 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akizungumza kuhusu uwajibikaji, weledi na uadilifu, Mhe. Masaju amewahimiza kuwajibika ipasavyo kama ambavyo imeelekezwa katika Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo unahimiza kuhusu uwajibikaji na kuweka wazi kuwa kila mtu ana wajibu wa kushiriki na kujituma kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji mali, kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale ya pamoja yaliyowekwa na sheria.

“Ibara ya 25 inatukumbusha kuhusu uwajibikaji, Ibara ya 25(1) inasema kwamba kazi pekee ndio huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa Wananchi na kipimo cha Utu...”

Ameongeza kuwa kazi ya kuhukumu waliyopewa sio ya shuruti hivyo wanapaswa kujituma wenyewe, kuwa na nidhamu ya kazi ili kufikia malengo na kuwa wazembe watashauriwa ili kubadilika au kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Hii kazi ya kuhukumu tuliyopewa si ya shuruti, ndio maana tunataka muwajibike mjitume ninyi wenyewe, muwe na nidhamu ya kazi, mfikie malengo, wale wazembe tutajaribu kuwashurutisha kwa kuwashauri, lakini ikishindikana watawawajibishwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao na tunayo sheria inatuongoza,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wapya aliowaapisha leo tarehe 04 Machi, 2026. Kulia ni Mhe. Moonlight Martin Tupa na kushoto ni Mhe. Deus Philo Nyimbo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto (wa kwanza kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kushoto), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Massabo (katikati), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma (wa pili kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe Abdi Kagomba (wa kwanza kulia) wakifuatilia tukio la uapisho wa Mahakimu Wakazi wapya (hawapo katika picha).

Mhe. Masaju amerejea Ibara ya 25(3)(d)(i)(ii)(iii) na kueleza kuwa, kazi ni majukumu yoyote ambayo ni sehemu ya majukumu ya kawaida ya kuhakikisha ustawi wa jamii, ujenzi wa Taifa kwa mujibu wa sheria pamoja na jitihada za kutumia uwezo wa kila mtu kufanya kazi kwa ajili ya kuimarisha jamii na uchumi wa Taifa na kuhakikisha maendeleo na tija ya Kitaifa.

Hafla ya Uapisho huo imehudhuriwa na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mahakimu Wakazi wengine 90 ambao walikuwa wakiendelea na mafunzo elekezi baada ya uapisho wao tarehe 23 Februari, 2026.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here