NA LWAGA MWAMBANDE
MATUMIZI ya baiskeli ni njia rahisi na nafuu inayochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya na maisha ya binadamu. Kuendesha baiskeli husaidia kuimarisha moyo, kupunguza hatari ya magonjwa kama shinikizo la damu na kisukari, pamoja na kuongeza nguvu za mwili.
Waziri Mkuu wa zamani wa Uholanzi,Mark Rutte ni miongoni mwa viongozi wa mfano ambaye katika uongozi wake alitumia baiskeli kwenda kazini,kushiriki vikao na hata kuondoka ofisini baada ya majukumu ya kila siku.(Picha na Mtandao).
Aidha, zoezi hili huchangia afya ya akili kwa kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza hali ya furaha. Katika maisha ya kila siku, baiskeli hupunguza gharama za usafiri na ni rafiki kwa mazingira kwa kuwa haitoi hewa chafu.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, kwa ujumla, matumizi ya baiskeli ni muhimu katika kujenga jamii yenye afya bora, uchumi nafuu na mazingira safi.Endelea;
1. Baiskeli nakwita, kokote kule uliko,
Ujue nakutafuta, uniambie uliko,
Nashindwa kupitapita, niweze kufika huko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
2. Baiskeli sikia, nimejua wema wako,
Ambao sikujulia, kwa wengine ni kicheko,
Kumbe kwa kukutumia, afya yawa na mashiko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
3. Pedeli nikikanyaga, nafika hadi Moroko,
Nakwenda na zangu swaga, na jasho ni bubujiko,
Viungo vishajitega, misuli ni changamko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
4. Nahesabu kilometa, mbiombio za mashiko,
Upepo mwema napata, si hewa ofisi huko,
Tena ninapitapita, bila ya foleni huko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
5. Kweli ninajilaumu, nilivyobakia huko,
Bila hata kufahamu, baiskeli mashiko,
Sasa nimeshafahamu, huu wako ni mwaliko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
6. Nawashauri wenzangu, afya za kwenu ziweko,
Igeni chaguo langu, pedeli tumia huko,
Huo wa kwenu uchungu, kwenu hautakuweko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
7. Baiskeli tokea, mbele kuna pate yako,
Pale ukitokezea, maandalizi ya ujiko,
Vema nitakupokea, hata chereko ziweko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
8. Ili kuijenga afya, baiskeli ziweko,
Tuache kupiga chafya, kikohozi kisiweko,
Hali inayoogofya, na hiyo haitakuweko,
Wewe wa muhimu sana, kwa afya na mazoezi.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
