DAR-Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Belarus, Mheshimiwa Maxim Ryzhenkov atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia Aprili 28 hadi 30, 2026 kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo Aprili 27,2026 imeeleza kuwa, akiwa nchini, Mheshimiwa Ryzhenkov atafanya mazungumzo ya uwili na mwenyeji wake Aprili 28, 2026 jijini Dar es Salaam pamoja na kukutana na viongozi wengine wa Serikali.
Lengo la ziara hii ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Belarus pamoja na kudumisha ushirikiano wa kirafiki katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, elimu, afya na teknolojia.
Aidha, ziara hii inalenga kuimarisha ushirikiano ushirikiano wa kibiashara kati ya sekta binafsi za nchi hizi mbili.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Belarus ulianzishwa mwaka 1996, na nchi hizi zimeendelea kuimarisha ushirikiano huo katika sekta mbalimbali.
Kuna fursa kubwa ya kupanua biashara kati ya nchi hizi mbili, ambapo Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuongeza mauzo yake katika soko la Belarus, hususan katika bidhaa zenye thamani ya juu kama kahawa ghafi, maua, na parachichi.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, Belarus imewekeza katika miradi mbalimbali nchini kupitia sekta za viwanda na miundombinu ya kiuchumi, yenye thamani ya dola za Marekani milioni 0.54, ambayo imechangia kuajiri Watanzania 78.
Vilevile, kuna fursa kubwa ya kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali,hususan kutokana na uzoefu wa Belarus katika kilimo, elimu, maendeleo ya rasilimali watu, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Ziara hii ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Belarus,inayotarajia kuimarisha mahusiano na urafiki uliopo pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano na uwekezaji utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
