BoT yawakutanisha wanachama wa AFI jijini Arusha kuboresha sera za fedha ziwe jumuishi

ARUSHA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaratibu mkutano wa kimataifa wa nchi wanachama wa Muungano wa Ujumuishaji wa Kifedha (AFI), unaofanyika jijini Arusha, ukiwa na lengo la kuboresha sera za fedha ili ziwe jumuishi zaidi.
Mkutano huo ulifunguliwa rasmi tarehe 11 Mei 2026 na Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, ambaye alisisitiza kuwa mkutano huo utakuwa suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia mijadala itakayofanyika.

Mkutano huo, unaotarajiwa kutamatika Alhamisi, tarehe 14 Mei 2026, umegawanyika katika vikundi kazi viwili: kimoja kikijikita katika Viwango vya Kimataifa vya Uwiano katika Sera (GSP), na kingine kikijadili Ufadhili kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEF).
Akizungumza katika ufunguzi huo, Bi. Msemo alisema kuwa mkutano huo unalenga kuangalia namna bora ya kusaidia wanawake na makundi maalum ya wajasiriamali kupitia sera jumuishi na kanuni rafiki.

Alibainisha kuwa katika nchi nyingi, wanawake wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa dhamana, haki za ardhi, pamoja na changamoto za ujumuishwaji wa kidijitali.
Licha ya changamoto hizo, Bi. Msemo alieleza kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika safari ya ujumuishi wa kifedha. Alifafanua kuwa kupitia Mfumo wa Taifa wa Ujumuishi wa Kifedha wa mwaka 2023–2028, malengo madhubuti yamewekwa na yanaendelea kutekelezwa katika maeneo ya upatikanaji, matumizi, ubora wa huduma na ustawi wa kifedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Programu na Utekelezaji wa AFI, Dkt. Eliki Boletawa, alisema kuwa ushirikiano kati ya nchi wanachama ni muhimu katika kuhakikisha kuwa sera za kifedha zinakuwa jumuishi zaidi na zinawafikia wananchi wengi zaidi.
Ikumbukwe kuwa, katika kuonesha mafanikio ya ujumuishi wa kifedha, mwaka 2025 BoT ilipokea tuzo ya ubunifu katika ujumuishi wa kifedha, inayojulikana kama Nestor Espenilla Jr. Award.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here