NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini kinyume na taratibu za kisheria.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Mei 13,2026 ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.Amesema,ukamataji huo ni matokeo ya operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa mwezi Aprili,2026.
"Kemikali zilizokamatwa ni Cyclohexanone zenye ujazo wa lita 16,048 pamoja na Extra Neutral Alcohol (ENA) zenye ujazo wa lita 50,000."
Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kupitia operesheni hiyo,magari mawili yaliyohusika katika usafirishaji wa kemikali hizo yanashikiliwa na watuhumiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Amesema,uchunguzi umebaini kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka husika.
Vilevile ameongeza kuwa,kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zikisafirishwa kwa kutumia magari ya mafuta aina ya Petrol yaliyokuwa yamebandikwa vibali vya kughushi, hali inayotajwa kuwa ni sehemu ya mtandao wa kihalifu unaolenga kuzichepusha kemikali hizo kwa matumizi haramu.
Kamishina Jenerali Lymo amesema kuwa, kemikali aina ya Cyclohexanone hutumika kuzalisha dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP) na kwamba kiasi kilichokamatwa kingeweza kuzalisha takribani tani 11.4 za dawa hizo haramu nchini.
"Kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya kuimarika duniani,mitandao ya kihalifu imekuwa ikitumia kemikali bashirifu kuzalisha dawa za kulevya katika maabara bubu," amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.
Amesema,kemikali hizo ni halali kwa matumizi mbalimbali ya viwandani, kitabibu, kilimo, ujenzi,madini pamoja na tafiti za kisayansi, lakini wahalifu huzitumia vibaya kwa kuzichepusha kutoka katika matumizi halali na kuzitumia kutengeneza dawa za
kulevya.
"Hali hiyo imeongeza changamoto katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya
duniani na kuifanya nchi yetu kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali
bashirifu ili kuzuia uchepushwaji wake katika matumizi haramu."
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)