NA ARON MSIGWA
Nairobi
MKURUGENZI wa Mafunzo na Elimu ya Jumla ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Beno Mathias Nzowa amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kushiriki zoezi la pamoja la 14 la Vituo vya Uamrishaji vya Kijeshi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - Ushirikiano Imara 2026, litakalofunguliwa rasmi Mei 14, 2026 katika viwanja vya Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, Kenya.
Kanali Nzowa amesema hayo baada ya kutembelea kikundi cha Tanzania kinachoshiriki zoezi hilo katika Kituo cha Mafunzo cha Masuala ya Usalama na Haki za Binadamu (HPSS) jijini Nairobi kwa lengo la kukagua maandalizi na utayari wa washiriki kuelekea uzinduzi rasmi wa zoezi hilo la kikanda lililowajumuisha Maofisa wa Jeshi, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto,Wizara na taasisi za kiraia.
"Nimekuja hapa kuangalia maandalizi kuelekea ufunguzi wa zoezi ambalo litafanyika kwa siku 14. Maandalizi ni mazuri na Kikosi chetu kutoka Tanzania kina utayari mkubwa pamoja na morali ya hali ya juu kutokana na maandalizi na mafunzo ya awali yaliyoelekezwa na Mkuu wa Majeshi kufanyika jijini Arusha,” amesema Kanali Nzowa.
Zoezi la Ushirikiano Imara 2026 linawakutanisha washiriki kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, usalama wa kikanda pamoja na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama.




