NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Marekani imetangaza kuanzishwa kwa operesheni kubwa ya kijeshi baharini yenye lengo la kurejesha usafirishaji wa kibiashara kupitia mlango wa Hormuz Strait, mojawapo ya njia muhimu zaidi za nishati duniani.
Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (US Central Command), operesheni hiyo iliyopewa jina la “Project Freedom” itatekelezwa kwa maelekezo ya rais, ikilenga kuhakikisha uhuru wa usafiri wa meli za kibiashara katika njia hiyo nyeti ya bahari.
Mlango wa Hormuz hupitisha takribani robo ya biashara ya mafuta duniani inayosafirishwa kwa njia ya bahari, sambamba na kiasi kikubwa cha bidhaa za mafuta na mbolea, hivyo kuifanya kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa dunia.
Njia hiyo ilifungwa kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, ambapo zaidi ya maeneo 17,000 yalilengwa katika kipindi cha wiki sita za mapigano.
Kwa kujibu mashambulizi hayo, Iran ilitekeleza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati, ikilenga mali zinazodaiwa kumilikiwa na Marekani hasa katika nchi za Ghuba ya Kiarabu pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.
Hali imeendelea kuwa tata kutokana na hatua za kulipizana kisasi katika usimamizi wa usafiri wa baharini ndani ya Mlango wa Hormuz, ambapo Iran imeimarisha udhibiti wa meli zinazopita, huku Marekani ikitekeleza hatua za kijeshi dhidi ya meli zinazohusishwa na bandari za Iran.
Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Kamanda wa CENTCOM, Brad Cooper ameeleza kuwa,msaada wa Marekani katika operesheni hiyo ya kujihami ni muhimu kwa usalama wa kikanda na uchumi wa dunia, hasa wakati nchi hiyo ikiendelea kudumisha mzingiro wa baharini.
Operesheni hiyo pia inaambatana na mpango mpana wa kidiplomasia na kiusalama uliotangazwa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi, unaojulikana kama “Maritime Freedom Construct”.
Mpango huo unalenga kuimarisha uratibu na ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia miongoni mwa washirika wa kimataifa ili kulinda usalama wa baharini katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa CENTCOM, msaada wa kijeshi wa Marekani katika operesheni hiyo utahusisha manowari zenye makombora ya kuongozwa, zaidi ya ndege 100 za kijeshi za ardhini na baharini, mifumo ya kisasa isiyo na rubani inayofanya kazi katika nyanja mbalimbali, pamoja na wanajeshi wapatao 15,000.
Tangazo la uzinduzi wa operesheni hiyo lilikuja saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kusema kuwa mazungumzo “yenye mwelekeo chanya” yanaendelea kati ya nchi yake na Iran kuhusu mzozo huo.
Aidha, alithibitisha kuwa vikosi vya Marekani vitaanza kusindikiza meli zilizokwama katika Mlango wa Hormuz chini ya operesheni hiyo.
Kupitia mtandao wa Truth Social, Trump aliielezea operesheni hiyo kama “hatua ya kibinadamu”, akidai kuwa baadhi ya meli katika eneo hilo zilikuwa zikikabiliwa na uhaba wa chakula, ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu namna mfumo wa usindikizaji utakavyotekelezwa.
Hata hivyo, tangazo hilo limeibua taharuki kutoka Iran. Afisa mwandamizi wa nchi hiyo ameonya kuwa hatua yoyote ya Marekani kuingilia kati usafiri wa baharini katika eneo hilo itachukuliwa kama ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Ebrahim Azizi, ambaye ni mkuu wa kamati ya usalama wa taifa ya bunge la Iran, aliandika kupitia mtandao wa X kwamba, “Uingiliaji wowote wa Marekani katika mfumo mpya wa usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz utachukuliwa kama uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.”
Wakati huo huo, shirika la utangazaji la ABC News limeripoti, likinukuu msemaji wa CENTCOM, kuwa meli ya Iran iliyokamatwa, Touska, pamoja na wafanyakazi wake, wamehamishiwa Pakistan kwa ajili ya kurejeshwa Iran. Kwa mujibu wa Tim Hawkins, jumla ya wafanyakazi 22 wa meli hiyo walikabidhiwa rasmi.
Tukio hilo linafuatia hatua ya Marekani ya Aprili 19, ambapo ilizuia na kuikagua meli ya mizigo ya Iran iitwayo Touska katika Ghuba ya Oman, ikiwa ni sehemu ya operesheni ya kusimamia shughuli za usafirishaji zinazohusishwa na Iran karibu na Mlango wa Hormuz.
Meli hiyo ilidaiwa kuelekea katika bandari ya Iran kabla ya kukamatwa na kuwekwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Marekani.
