NA DIRAMAKINI
RIPOTI mpya zinaonesha kuendelea kuwepo kwa hali ya sintofahamu kuhusu mabadiliko ya udhibiti wa eneo la kimkakati la Mlango-Bahari wa Hormuz, huku mvutano wa kijeshi kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuathiri sekta ya usafirishaji wa baharini.
Taswira ya ramani inayodaiwa kutolewa na IRGC.Picha na Mtandao.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kupitia kikosi chake cha majini, limetoa ramani mpya inayoainisha eneo linalodaiwa kuwa chini ya udhibiti wake katika mlango huo muhimu wa bahari.
Kwa mujibu wa ramani hiyo, mpaka wa Magharibi unaanzia katika mstari unaounganisha ncha ya Magharibi kabisa ya Kisiwa cha Qeshm cha Iran na Imarati ya Umm al-Qaiwain ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kwa upande wa Mashariki, eneo hilo linaishia katika mstari unaounganisha Mlima Mobarak wa Iran na Imarati ya Fujairah.
Hata hivyo, haijabainika wazi ikiwa au kwa kiwango gani eneo hilo la udhibiti lililodaiwa limebadilika ukilinganisha na hali ya awali.
Katika maendeleo yanayohusiana, hakukuwa na ongezeko la wazi la shughuli za meli katika Mlango wa Hormuz kufikia Jumatatu, siku moja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza kuwa nchi yake ingeanza juhudi za kuhakikisha uhuru wa usafiri wa baharini katika eneo hilo.
Takwimu kutoka mfumo wa ufuatiliaji wa meli wa MarineTraffic zinaonesha kuwa, ni meli moja tu ya kusafirisha gesi ya LPG ambayo iko chini ya vikwazo, pamoja na meli chache za mizigo na meli ya kuweka nyaya baharini, ndizo zilizopita kuelekea Ghuba ya Oman siku hiyo.
Aidha, hakukuonekana na foleni ya meli za kibiashara au meli za mafuta zikisubiri kuvuka, huku kampuni ya usafirishaji ya Ujerumani, Hapag-Lloyd, ikieleza kuwa bado haiwezekani kwa meli zake kupita kutokana na ukosefu wa mwongozo ulio wazi kuhusu taratibu za usalama wa njia.
Kwa upande wake, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilitangaza kuanza kusaidia kurejesha uhuru wa usafiri katika mlango huo huku ikiendelea na hatua zake za kuzuia shughuli katika bandari za Iran.
Hata hivyo, Baraza la Kimataifa la Usafirishaji wa Baharini (BIMCO) limesema kuwa, sekta hiyo bado haijapokea mwongozo wowote rasmi kuhusu operesheni ya Marekani, na kusisitiza kuwa hali ya usalama kwa ujumla haijabadilika.
Afisa Mkuu wa Usalama wa BIMCO, Jakob Larsen alieleza kuwa,bila ridhaa ya Iran kuruhusu meli za kibiashara kupita kwa usalama, bado haijulikani iwapo tishio dhidi ya meli linaweza kupunguzwa au kudhibitiwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Usafirishaji wa Baharini (IMO), mamia ya meli za kibiashara pamoja na mabaharia 20,000 wameshindwa kutumia njia hiyo kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Iran, Marekani, Israel na washirika wake.
Kituo cha Pamoja cha Taarifa za Usalama wa Baharini kinachoongozwa na Marekani kimeendelea kuainisha kiwango cha tishio katika Mlango wa Hormuz kuwa ni “hatari kubwa,” kikishauri mabaharia kutumia njia mbadala kupitia maji ya Oman kusini mwa njia rasmi ya usafiri wa meli.
Wakati huohuo, Iran imeonya Jeshi la Wanamaji la Marekani kutoingia katika eneo hilo na kusisitiza kuwa meli zote za kibiashara zinapaswa kuratibu safari zao na vikosi vyake vya kijeshi. Nchi hiyo pia imetoa ramani mpya inayobainisha kile inachodai kuwa ni mipaka ya udhibiti wake.
Katika hatua nyingine, Pakistan imethibitisha kuwa wafanyakazi wote 22 wa meli ya mizigo ya Touska yenye bendera ya Iran, waliokamatwa mwezi uliopita na vikosi vya Marekani, wamehamishwa kwenda Pakistan na wanatarajiwa kurejeshwa makwao.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imeeleza kuwa,meli hiyo pia itarejeshwa kwa wamiliki wake baada ya kufanyiwa matengenezo, ikitaja hatua hiyo kuwa ni juhudi ya kujenga imani.
Wakati huo huo, zuio la kijeshi la majini lililowekwa na Marekani katika bandari za Iran tangu Aprili 13 limeendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa mauzo ya mafuta ya nchi hiyo, hali inayoweza kuwa na athari pana kwa uchumi wa kimataifa.(NA)
