NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amempokea Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa William Samoei Ruto, Ikulu jijini Dar es Salaam, aliyewasili nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili.
Rais Dkt.Samia na mgeni wake wamefanya mazungumzo ya faragha na kuongoza mazungumzo rasmi ya pande mbili, kisha kushuhudia utiwaji saini wa mikataba nane kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala waliyojadili ya kuimarisha ushirikiano katika biashara, uwekezaji, nishati, kilimo, miundombinu, utalii, Tehama, ulinzi na usalama.
Marais hao wamekubaliana kuongeza kasi ya kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili, wakidhamiria kumaliza vikwazo vilivyosalia ifikapo mwisho wa Mei, 2026.
Aidha, wamekubaliana kuimarisha Kamati za Pamoja za Biashara zitakazokutana mara kwa mara kushughulikia changamoto zilizopo na kuzuia kuibuka kwa vikwazo vipya vinavyoweza kuathiri biashara baina ya nchi hizo.Katika nishati na miundombinu, Tanzania na Kenya zimejadili miradi ya kuunganisha mifumo ya umeme, bomba la gesi asilia, reli kupitia Tanga, Moshi, Kilimanjaro na Taveta, pamoja na ukanda wa barabara ya Dar es Salaam, Bagamoyo, Pangani, Tanga, Horohoro hadi Mombasa.
Rais Ruto amesema,Tanzania na Kenya ni nchi zinazohitajiana na kutegemeana, na kwamba uhusiano wake unapaswa kujengwa katika kuondoa mashaka, kuweka madaraja ya kibiashara na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wa pande zote mbili.
Ameongeza kuwa, biashara kati ya Tanzania na Kenya ilifikia dola za Marekani milioni 860 mwaka 2025, na ingeweza kuvuka dola bilioni moja endapo vikwazo visivyo vya kikodi visingeathiri mtiririko wa biashara kati ya nchi hizo mbili.Katika hatua nyingine, viongozi hao wameshuhudia utiaji saini wa mikataba na hati nane za makubaliano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kenya, katika maeneo ya reli, upembuzi yakinifu wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, usaidizi wa kisheria katika makosa ya jinai, kilimo, utambuzi wa vyeti vya mabaharia, usimamizi wa usafiri wa majini, viwango kati ya Zanzibar na Kenya, pamoja na kujengeana uwezo katika utumishi wa umma.
Vilevile, Rais Dkt.Samia na Rais Ruto wameshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Tanzania na Kenya, lililowakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji na sekta binafsi kutoka nchi zote mbili.
Akifunga kongamano hilo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania itaendelea kufanya kazi na Kenya katika kuondoa vikwazo vya biashara, kurekebisha sheria na mifumo inayokwamisha uwekezaji, pamoja na kujenga miundombinu ya kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, Rais Ruto amesema Tanzania na Kenya zinaweza kufikisha thamani ya biashara ya hadi dola za Marekani bilioni moja na kuvutia uwekezaji mpya wa kuvuka mipaka wa dola milioni 500 ndani ya miaka mitatu, endapo zitaondoa vikwazo na kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi.Katika kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya wamewasilisha uzoefu wa uwekezaji wa pande mbili na kueleza haja ya kuongeza ushirikiano katika viwanda, nishati, fedha, kilimo, miundombinu na huduma.








