NA DIRAMAKINI
JESHI la Anga la Falme za Kiarabu limeripotiwa kufanya mashambulizi ya siri dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Iran, likiwemo shambulizi dhidi ya kiwanda cha kusafisha mafuta katika Kisiwa cha Lavan kilichopo kwenye Ghuba ya Uajemi.
Taarifa hiyo imeibua taharuki mpya ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati huku mvutano kati ya Tehran na mataifa ya Ghuba ukiendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, mashambulizi hayo yamefanyika kipindi ambacho juhudi za kusitisha mapigano kati ya Iran, Marekani na washirika wake zilikuwa zinaendelea.
Vyanzo vya kiintelijensia vilivyonukuliwa na gazeti la Wall Street Journal vimedai kuwa, ndege za kijeshi za UAE zilihusika moja kwa moja katika operesheni hiyo ya siri.
Mashambulizi hayo yalidaiwa kusababisha moto mkubwa katika kiwanda hicho cha mafuta cha Lavan Island, hali iliyosababisha sehemu kubwa ya uzalishaji kusimamishwa.
Serikali ya Iran ilikiri kutokea kwa shambulizi hilo,lakini haikutaja rasmi taifa lililohusika wakati huo, ikieleza kuwa tukio hilo lilifanywa na “maadui wa taifa.”
Baada ya tukio hilo, Iran ilidai kujibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea UAE pamoja na Kuwait.
Ripoti zinaonesha kuwa,tangu kuanza kwa mzozo huo, UAE imekuwa moja ya mataifa yaliyolengwa zaidi na mashambulizi ya Iran, hasa kutokana na uhusiano wake wa karibu na Marekani na ushirikiano wake wa kiusalama na Israel.
Wachambuzi wa masuala ya kijeshi na siasa za Mashariki ya Kati wanaeleza kuwa,hatua ya UAE kuhusishwa moja kwa moja katika mashambulizi dhidi ya Iran ni ishara ya mabadiliko makubwa ya sera ya kiusalama ya Abu Dhabi.
Kwa miaka mingi, UAE ilikuwa ikijaribu kujiepusha kuingia moja kwa moja kwenye migogoro ya kijeshi dhidi ya Iran licha ya tofauti zao za kisiasa na kiitikadi.
Hata hivyo, kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu yake ya nishati na uchumi kunaonekana kuilazimisha nchi hiyo kuchukua hatua kali zaidi za kijeshi.
Mvutano huo pia umeibua hofu kuhusu usalama wa usafirishaji wa mafuta katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Hormuz, eneo muhimu kwa biashara ya mafuta duniani.
Aidha,wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa, kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta kunaweza kusababisha kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia pamoja na kuyumbisha uchumi wa mataifa yanayotegemea nishati kutoka Mashariki ya Kati.
Hadi sasa, serikali ya UAE haijatoa tamko rasmi kuthibitisha kuhusika kwake katika mashambulizi hayo. Hata hivyo, baadhi ya maafisa wa nchi hiyo wamekariri kuwa UAE ina haki ya kujilinda dhidi ya vitisho vya nje vinavyolenga usalama wa taifa na miundombinu yake muhimu. (NA)
