Profesa Shemdoe aielekeza Kampuni ya CRBC kukamilisha ujenzi wa barabara saba Ubungo ifikapo Agosti 14,2026

DAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI),Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ametaka Mkandarasi kampuni ya China Railways and Bridges Corporation (CRBC) inayojenga barabara tisa (9) za lami zenye urefu wa kilometa 5.42 kukamilisha ujenzi wa barabara saba (7) zilizosalia ifikapo Agosti 14, 2026, barabara hizo zinajengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) katika kata za Sinza, Mburahati, Mabibo na Makurumla wilayani Ubungo.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Juni 13, 2026 Katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa barabara 23 zenye urefu wa kilometa 52.37 zinazojengwa wilayani Ubungo katika kata 11 kupitia utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II).

Prof. Shemdoe amesitiza kuwa, mkandarasi huyo anayesuasua katika ujenzi wa barabara hizo kwa kisingizio cha lami kuchelewa kufika kutokana na vita ya Mashariki ya Kati, hatopewa muda wa nyongeza wa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo iwapo atashindwa kukamilisha ifikapo Agosti 14, 2026 kwa mujibu wa mkataba.
“TARURA hakuna kumuongezea muda mkandarasi huyu, atafute lami popote atakapoipata na afanye kazi usiku na mchana kukamilisha barabara hizi 7 zilizosalia ili kuwaondolea adha wananchi,”amesisitiza Prof. Shemdoe.

Katika kuhakikisha barabara zinakamilika kwa wakati, Prof. Shemdoe ameitaka TARURA na Mshauri Elekekezi (NIMETA Consult (T) kumshauri mkandarasi CRBC kwa kuangalia uwezekano wa kukabidhi baadhi ya barabara hizo kwa mkandarasi mwingine (sub contract) ili ujenzi ukamilike kwa wakati.

Aidha, Prof. Shemdoe amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff kumuondoa Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Bw. Evans Mgeusa anayesimamia Fedha za Miradi ya Benki ya Dunia kwa kitendo cha kuchelewesha malipo na kumleta mwingine ambaye atafanya kazi kwa weledi na wakati.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI), Bw. Adolf Ndunguru kuwaondoa Wahasibu Bw. Julius Bashuta na Mbwana Mkembe wa kitengo hicho cha Fedha na Uhasibu kinachosimamia fedha za miradi ya Benki ya Dunia, na kuwaleta wengine ambao watafanya kazi vizuri na kwa uaminifu.
Akizungumzia jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, Prof. Shemdoe amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utiaji saini wa mikataba minne ya ujenzi wa barabara za wilaya ya Ubungo yenye thamani ya shilingi bilioni 77, 457,169,172.73 kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II).

Kwa upande wake Mkazi wa Sinza,Bw. Jawa Waziri amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kufanya ziara ya ukaguzi wa barabara ya mtaa wake wa Sinza Lion na kumpongeza kwa kumuelekeza mkandarasi CRBC kukamilisha kwa wakati barabara hiyo ambayo imekuwa ni kero kwa wakazi wa eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here