DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza taasisi za umma kutathminiwa kwa kuzingatia tija ya uwekezaji, ubora wa huduma, uwezo wa kujitegemea na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo, Ikulu Dar es Salaam, wakati wa hafla ya Siku ya Gawio 2026 iliyobeba kaulimbiu isemayo, “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu kuelekea Dira 2050,” ambapo amepokea gawio na michango yenye thamani ya shilingi trilioni 1.327 kutoka kwa mashirika, taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
Amesema ongezeko la gawio la mwaka huu limetokana na kuimarika kwa tija, uzalishaji na ufanisi wa taasisi za umma, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hayapaswi kupimwa kwa gawio pekee bali pia kwa ubora wa huduma, uwezo wa kujitegemea namchango wake katika ukuaji wa uchumi.
Rais Dkt. Samia pia ameagiza taasisi zilizoshindwa kutoa gawio, zilizotoa pungufu au zilizopunguza kiwango cha gawio zikilinganishwa na mwaka uliopita kufanyiwa tathmini ili kubaini sababu za mwenendo huo na kuchukua hatua stahiki.
Aidha, amezitaka wizara, bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kusimamia kwa karibu utendaji wa taasisi zilizo chini yao, akisisitiza kuwa uwajibikaji na tija si jukumu laOfisi ya Msajili wa Hazina pekee.
Pia ameielekeza Ofisi hiyo kuendelea kusimamia uwekezaji wa Serikali ili ulete manufaa yanayolingana na thamani ya umiliki wa Serikali. Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Dkt. Samia amesema utekelezaji wake unahitaji taasisi zenye nidhamu, uadilifu, ubunifu na utendaji unaopimwa kwa matokeo badala ya mazoea.
“Hatutaweza kujenga uchumi shindani kwa taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea.Tunahitaji taasisi zinazopimwa kwa matokeo badala ya takwimu pekee,” amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha, amezipongeza taasisi zilizoongeza gawio, zilizorejea kwenye faida na zilizopunguza utegemezi wa ruzuku, akisema hatua hiyo inaashiria kuimarika kwa utendaji wa taasisi za umma.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, amesema mafanikio hayo yanatokana na mageuzi ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kupitia falsafa ya 4R na kuifungua nchi, hatua iliyoweka msingi imara wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amesema taasisi 14 kati ya308 zimetunukiwa kwa kufanya vizuri katika utoaji wa gawio na michango kwa Mfuko Mkuu wa Serikali.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia pia alitunukiwa Tuzo Maalum ya “Kinara wa Mageuzi katika Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Mashirika ya Umma kwa Maendeleo Jumuishi na Ustawi wa Taifa – Gawio Day 2026,” kwa mchango wake katika kuimarisha usimamizi wa uwekezaji wa umma na kuongeza tija ya taasisi za Serikali.
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
Gawio Day
Gawio Day 2026
Gawio la Serikali
Habari
Ofisi ya Msajili wa Hazina
