TAMISEMI yatoa ufafanuzi kuhusu pendekezo la treni ya mapema ya SGR kati ya Dar na Dodoma

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) imetoa ufafanuzi kuhusu mjadala unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusiana na pendekezo la Waziri Profesa Riziki Shemdoe la kuanzishwa kwa huduma ya treni ya kisasa ya SGR ya mapema alfajiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 30,2026 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-TAMISEMI, Roida Andusamile.

Ameeleza kuwa, pendekezo hilo limetafsiriwa tofauti na kusudio lake halisi, huku ikisisitiza kuwa lengo lake ni kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi wote na si kwa watumishi wa umma pekee.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Profesa Shemdoe alitoa pendekezo hilo alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa 2026, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Uchukuzi.

Katika maelezo yake, Waziri huyo alibainisha kuwa,kuna mahitaji ya wananchi ya kuwepo kwa safari za mapema alfajiri za treni ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, ili kuwawezesha wasafiri kufika mapema katika maeneo yao ya shughuli.

OWM-TAMISEMI imefafanua kuwa,huduma hiyo ingeweza kuwasaidia wananchi wanaosafiri kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, zikiwemo kuhudhuria mikutano, kupata huduma za Serikali na sekta binafsi, kufanya biashara, kuhudhuria matibabu, masomo pamoja na shughuli nyingine muhimu.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa,Profesa Shemdoe alitumia mfano wa baadhi ya watumishi wa umma ambao wenza wao wanafanya kazi katika miji tofauti, hususan pale ambapo taasisi zao hazina ofisi katika miji yote miwili.

Imefafanuliwa kuwa,mfano huo ulitumika kuelezea uhitaji uliopo katika jamii na haukuwa na maana ya kwamba huduma hiyo inalenga kuwahudumia watumishi wa umma pekee.

“TAMISEMI inapenda kusisitiza kuwa pendekezo hilo lilikuwa na lengo la kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi wote wenye mahitaji ya kusafiri mapema kati ya Dar es Salaam na Dodoma, badala ya kundi maalumu la watumishi wa umma,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa,huduma za treni za mapema katika miji mikubwa ni jambo la kawaida katika nchi nyingi zenye mifumo ya kisasa ya reli, na kwamba Tanzania, kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, inaendelea kupanua huduma za reli ya kisasa ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Aidha,OWM-TAMISEMI imewataka wananchi kuupokea mjadala huo kwa kuzingatia muktadha halisi wa pendekezo hilo na kupuuza tafsiri zinazopotosha dhamira ya kuboresha huduma za usafiri kwa manufaa ya wananchi wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here