TAKUKURU yawafikisha mahakamani watumishi tisa Geita kwa ubadhirifu

GEITA-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, imewafikisha mahakamani watumishi tisa wa umma kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali na kuisababishia hasara Serikali zaidi ya Shilingi milioni 90.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, watumishi watatu wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa Shilingi 48,067,500 zilizokusanywa kupitia mfumo wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS).

Ni kwa kutumia mashine za kukusanyia mapato (POS), lakini Fedha hizo hazikuwasilishwa katika akaunti ya serikali kinyume na taratibu.

Watuhumiwa hao ni Afisa Umwagiliaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Ally Hasan Semfukwe, Afisa Mifugo, Edward Cloward, pamoja na Mkusanya Mapato, Happyness Regnes Mushi.

Katika tukio lingine, TAKUKURU imewafikisha Mahakamani Watumishi wanne wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita kwa tuhuma za ubadhirifu wa Shilingi 41,987,607.50 kutoka akaunti ya mirathi ya Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Geita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwalipa watu wawili ambao hawakuwa na madai ya Mirathi, kisha fedha hizo kurejeshwa kwa njia ya miamala ya Benki na simu katika kile kilichoelezwa kuwa ni mpango wa “kickback”.

Watuhumiwa katika shauri hilo ni Afisa Hesabu Mkuu, Bulemo Yuda Mswaga, Msaidizi wa Hesabu, Mercy Geoffrey Magezi, Mhasibu Baldo Donatus Kafene na dereva William John Mbwambo.

Aidha, TAKUKURU imeeleza kuwa Watuhumiwa hao walishirikiana na Watumishi wengine kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ambao ni Fundi Sanifu wa Chuo cha Utafiti wa Madawa Mwanza, Mernad Mernad Mbena, na Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, David Thomas Moshy.

Kwa mujibu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, watuhumiwa wote wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita Juni 17, 2026 na kufunguliwa mashauri manne yanayohusiana na tuhuma hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here