NA GODFREY NNKO
TANZANIA imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa 62 wa Magavana wa Benki Kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika jijini Dar es Salaam, huku viongozi hao wakijadili mikakati ya kuimarisha uthabiti wa uchumi wa ukanda huo katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi.
Akifungua mkutano huo leo Juni 11, 2026, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema,mkutano huo ni sehemu ya vikao vinavyofanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kutathmini mwenendo wa uchumi,masuala ya fedha na mifumo ya kifedha katika nchi wanachama wa SADC.
Amesema,nchi zote 16 zinazounda SADC zimeshiriki katika mkutano huo, pamoja na taasisi mbalimbali za kifedha za kimataifa na kikanda, zikiwemo International Monetary Fund (IMF), wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii, bima na taasisi zinazohusika na ujumuishaji wa huduma za kifedha.
"Tumekutana kujadili mwenendo wa uchumi wa ukanda wetu na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa. Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu unaowakutanisha watunga sera za fedha kutoka mataifa yote ya SADC,”amesema Tutuba.
Gavana Tutuba amesema,moja ya ajenda kuu za mkutano huo ni kujadili namna nchi za SADC zinavyoweza kujikinga dhidi ya misukosuko ya uchumi wa dunia ambayo imekuwa ikiathiri mataifa mengi kupitia kupanda kwa gharama za maisha, mfumuko wa bei, migogoro ya kisiasa, changamoto za nishati na kuyumba kwa masoko ya fedha.
Amesema,washiriki wa mkutano huo wanatathmini athari zinazoweza kujitokeza iwapo nchi za ukanda huo hazitachukua hatua za mapema katika kusimamia sera za fedha na mifumo ya kifedha.
“Dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Tumeona baadhi ya nchi zikikabiliwa na viwango vikubwa vya mfumuko wa bei na changamoto za ukwasi wa fedha. Hivyo ni muhimu kwa nchi za SADC kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha uthabiti wa uchumi wa ukanda wetu,”amesema.
Gavana Tutuba amesema,mkutano huo pia unajadili namna ya kuimarisha mifumo ya malipo ndani ya ukanda wa SADC ili kuhakikisha uhamishaji wa fedha unafanyika kwa usalama,haraka na kwa gharama nafuu.Amesema,viongozi hao wanatafakari mbinu za kuongeza ukwasi wa fedha katika mifumo ya kifedha bila kusababisha ongezeko la mfumuko wa bei.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, moja ya majukumu makubwa ya benki kuu ni kuhakikisha fedha zinapatikana kwa kiwango kinachohitajika ili kuchochea shughuli za uzalishaji na biashara, huku zikidhibitiwa kwa uangalifu ili zisichochee ongezeko la bei za bidhaa na huduma.
“Tunatumia zana mbalimbali za sera ya fedha kuhakikisha fedha zinafika kwenye shughuli za kiuchumi zinazohitajika bila kuleta shinikizo la mfumuko wa bei. Hili ni eneo muhimu sana katika usimamizi wa uchumi wa kisasa."
Akizungumzia hali ya uchumi wa Tanzania, Gavana Tutuba amesema nchi imeendelea kufanya vizuri katika kudhibiti mfumuko wa bei ikilinganishwa na baadhi ya mataifa mengine duniani.
Ameeleza kuwa, kabla ya changamoto za hivi karibuni katika soko la mafuta na mazingira ya kimataifa, kiwango cha mfumuko wa bei nchini kilikuwa wastani wa asilimia 3.2 katika robo ya kwanza ya mwaka.Hata hivyo, amesema kumekuwapo na dalili za ongezeko dogo la mfumuko wa bei, lakini Benki Kuu inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kiwango hicho kinaendelea kubaki ndani ya lengo la taifa la kati ya asilimia 3 na 5.
“Kwa sasa tupo karibu na asilimia nne, lakini bado tunaendelea kutumia zana mbalimbali za sera ya fedha kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya kiwango kinachokubalika na kinachowezesha uchumi kukua kwa utulivu,” amesema.
Amesisitiza kuwa,udhibiti wa mfumuko wa bei ni muhimu kwa sababu unapoongezeka kupita kiasi huathiri thamani ya fedha na uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha.
Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mazingira ya uchumi yanabaki kuwa rafiki kwa uwekezaji, biashara na uzalishaji.
Amebainisha kuwa,matarajio ya Tanzania kwa mwaka 2026 ni kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 6.3, kiwango ambacho kitategemea ufanisi wa mifumo ya malipo, upatikanaji wa mikopo, uthabiti wa sekta ya fedha na utekelezaji wa sera bora za uchumi.“Tunaendelea kuhakikisha mifumo ya malipo inafanya kazi kwa ufanisi, fedha zinawafikia wananchi kwa wakati, mikopo inapatikana kwa viwango vinavyokubalika na shughuli za uzalishaji zinaendelea kuchochewa katika sekta zote za uchumi,”amesema.
Katika mkutano huo, suala la ukwasi wa benki pia limepewa kipaumbele, huku magavana wakijadili namna ya kuhakikisha taasisi za kifedha zinakuwa na uwezo wa kutoa mikopo kwa wananchi na wafanyabiashara bila kuathiri uthabiti wa mfumo wa fedha.
Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu itaendelea kusimamia kwa karibu hali ya ukwasi katika sekta ya benki ili kuhakikisha huduma za kifedha zinapatikana kwa wakati na kwa masharti yanayokidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi.
Pia amezungumzia suala la viwango vya ubadilishanaji fedha za kigeni, akisema Tanzania imeendelea kudumisha utulivu katika eneo hilo kwa kuzingatia misingi ya soko.
Amesema,Benki Kuu inaendelea kusimamia kwa karibu benki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa viwango vya ubadilishanaji fedha. Viwango hivyo vinaendelea kuakisi nguvu za soko na hali imeendelea kuwa tulivu,”amesema.
Gavana Tutuba amesema,Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mbalimbali ya usimamizi wa sera za fedha, mifumo ya malipo na usimamizi wa sekta ya fedha ndani ya ukanda wa SADC.
Amebainisha kuwa,wataalamu kutoka Tanzania wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa uzoefu na mafunzo kwa nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo.
“Tunajivunia mafanikio ambayo tumeyapata katika usimamizi wa uchumi na sekta ya fedha. Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazotoa mchango mkubwa katika mijadala ya kiuchumi ndani ya SADC, na nchi nyingi zinakuja kujifunza kutoka kwetu,”amesema.Aidha,mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa kwa maazimio na mikakati mipya itakayolenga kuimarisha ushirikiano wa nchi za SADC katika kusimamia sera za fedha, kuimarisha mifumo ya malipo, kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha ukuaji endelevu wa uchumi katika ukanda huo.









