NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yatakayofanyika Juni 12, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Miaka 60 ya Kuendeleza Ustawi wa Kiuchumi: Kukuza Ubunifu, Mageuzi na Ustahimilivu”, yakilenga kuangazia mchango wa Benki Kuu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Juni 11, 2026, kando ya Mkutano wa 62 wa Magavana wa Benki Kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema,maadhimisho hayo ni tukio muhimu la kihistoria linalobeba mafanikio makubwa ya taasisi hiyo katika kusimamia uchumi wa taifa kwa kipindi cha miongo sita.
Gavana Tutuba amesema,Tanzania imepokea magavana wa benki kuu kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambao wamekaribishwa kushiriki katika maadhimisho hayo, akieleza kuwa ushiriki wao unaonesha umuhimu wa Tanzania katika masuala ya usimamizi wa uchumi na sekta ya fedha ndani ya ukanda huo.
Amesema,Benki Kuu ilianzishwa rasmi mwaka 1966 chini ya uongozi wa Rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikiwa na jukumu la kusimamia sera za fedha, kudhibiti mfumuko wa bei, kuchapisha na kusambaza fedha pamoja na kuhakikisha mfumo wa kifedha nchini unaendelea kuwa imara.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, safari ya miaka 60 ya BoT imeambatana na mageuzi makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia yaliyobadilisha namna wananchi wanavyofanya miamala ya kifedha.
Ameeleza kuwa,wakati wa kuanzishwa kwa Benki Kuu, matumizi ya fedha taslimu yalitawala kwa kiwango kikubwa huku baadhi ya maeneo yakiendelea kutumia mfumo wa kubadilishana bidhaa kwa bidhaa.
Hata hivyo, Tanzania imepiga hatua kubwa hadi kufikia matumizi ya mifumo ya kisasa ya malipo inayorahisisha shughuli za kiuchumi.
“Leo hii tuna mifumo ya kisasa ya malipo inayowawezesha wananchi kufanya miamala kwa urahisi zaidi kupitia simu za mkononi, matumizi ya TanQR na mfumo wa Tanzania Instant Payment System (TIPS), ambao umeunganisha huduma mbalimbali za kifedha na kurahisisha uhamishaji wa fedha kwa wakati halisi,”amesema Gavana Tutuba.
Ameongeza kuwa,maboresho hayo yameongeza ufanisi katika sekta ya fedha na kupunguza muda wa kushughulikia miamala mbalimbali ikiwemo uthibitishaji wa hundi.
“Zamani mchakato wa uthibitishaji wa hundi ungeweza kuchukua zaidi ya mwezi mmoja, lakini kutokana na maboresho ya mifumo ya kifedha, huduma hiyo sasa inaweza kukamilika ndani ya muda mfupi sana. Hii ni sehemu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya fedha nchini,”amesema.
Gavana Tutuba amesema,mafanikio ya Benki Kuu hayaonekani tu katika maendeleo ya mifumo ya malipo bali pia katika usimamizi wa uchumi wa taifa, ambao umeendelea kuonesha uimara licha ya changamoto mbalimbali za kimataifa.
Amebainisha kuwa,mwaka 2025 uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9, kiwango kilichozidi wastani wa ukuaji wa uchumi duniani uliokuwa asilimia 3.2.
Aidha, amesema kiwango cha mfumuko wa bei nchini kiliendelea kuwa katika hali ya utulivu kwa wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2025, ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 4.3.
“Matokeo haya yanaonesha uimara wa sera zetu za fedha na usimamizi wa uchumi kwa ujumla. Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi na kwa uthabiti,” amesema.
Kwa upande wa thamani ya sarafu, Tutuba amesema Shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa himilivu licha ya changamoto za kiuchumi zinazozikabili nchi nyingi duniani.
Amefafanua kuwa,katika mwaka ulioishia Machi 2026, thamani ya Shilingi ilishuka kwa wastani wa asilimia tatu pekee, tofauti na baadhi ya sarafu za mataifa mengine ambazo ziliporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 kutokana na misukosuko ya uchumi wa dunia.
Katika sekta ya benki, Gavana Tutuba amesema, Benki Kuu imeendelea kuimarisha usimamizi wa taasisi za kifedha ili kuhakikisha zinachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesema, kwa sasa Tanzania ina benki 42 zinazofanya kazi ya kutoa huduma za kifedha kwa wananchi na sekta mbalimbali za uzalishaji, hali inayochochea uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi.
Gavana Tutuba pia ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti mikopo chechefu, akisema hadi kufikia Machi mwaka huu kiwango cha mikopo hiyo kilikuwa asilimia 2.9, chini ya kiwango cha kimataifa cha asilimia tano kinachokubalika.
“Kiwango hiki kinaashiria kuwa sekta ya fedha nchini ipo katika hali nzuri. Watu wengi wanaokopa wana uwezo wa kurejesha mikopo yao kwa wakati, jambo linaloonesha mazingira mazuri ya biashara na uimara wa shughuli za kiuchumi,”amesema.
Akizungumzia maadhimisho hayo, amesema baada ya hafla ya ufunguzi itakayofanywa na Rais Dkt.Samia, kutafanyika kongamano maalumu litakalowakutanisha wataalamu wa uchumi, sekta ya fedha, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali kujadili mustakabali wa uchumi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Tutuba, kongamano hilo litakuwa na mada kuu mbili. Mada ya kwanza itajadili namna uchumi unavyoweza kuimarisha maisha ya wananchi na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kivita, ushuru wa biashara na misukosuko ya masoko ya dunia.
Mada ya pili itajikita katika nafasi ya teknolojia za kifedha (FinTech), mifumo ya kidijitali na matumizi ya akili unde katika kuimarisha huduma za kifedha, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Gavana Tutuba pia ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika maadhimisho hayo ya kihistoria, akisisitiza kuwa Benki Kuu imekuwa taasisi inayogusa maisha ya kila Mtanzania kupitia usimamizi wa fedha, sera za uchumi na mifumo ya malipo.
“Tunapoadhimisha miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania, tunajivunia mchango mkubwa uliotolewa katika kuimarisha uchumi wa taifa. Huu ni wakati wa kutafakari tulipotoka, tulipo na tunakoelekea,tunahaihidi kuendelea kubuni na kuboresha huduma zetu kwa manufaa ya Watanzania na maendeleo ya nchi kwa ujumla,”amesisitiza Gavana Tutuba.
