Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma kuanza kutumika Septemba 2026

DODOMA-Serikali imesema,Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika ndani ya mwezi Septemba,mwaka huu, hatua inayotarajiwa kuimarisha usafiri wa anga na kulipa hadhi zaidi jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya nchi.
Akizungumza wakati alipotembelea na kuona maendeleo ya mradi huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema, ujenzi wa uwanja huo umefikia hatua za mwisho ambapo miundombinu mikubwa ikiwemo njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na maeneo ya maegesho ya ndege imekamilika kwa kiwango kikubwa.

Mhe. Balozi Omar amesema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2022 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Afrika Growing Together Fund (AGTF), ukiwa na lengo la kujenga uwanja wa kisasa utakaoendana na mahitaji ya Mji Mkuu wa nchi.
"Dodoma ni makao makuu ya nchi, hivyo ilikuwa muhimu kuwa na uwanja wa ndege wa kisasa unaoweza kukidhi ongezeko la shughuli za kiuchumi, kiserikali na kijamii,”amesema Mhe. Balozi Omar.

Ameongeza kuwa,kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliyotolewa na watalaamu, sehemu ya kwanza inayohusisha miundombinu ya uwanja imefikia asilimia 86.73 ya utekelezaji, huku sehemu ya pili inayohusisha majengo muhimu ikiwemo jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege na jengo la zimamoto ikiwa imefikia asilimia 75.1.

“Uwanja huu utakuwa miongoni mwa viwanja vikubwa nchini, ukiwa na njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita 60, pamoja na maegesho makubwa ya ndege yatakayowezesha kuhudumia ndege nyingi kwa wakati mmoja,” ameongeza Mhe.Balozi Omar.
Aidha,Mhe.Balozi Omar amesema,kukamilika kwa uwanja huo kunatarajiwa kuufungua zaidi mji wa Dodoma kwa safari za ndani na kimataifa, huku ukiongeza mvuto wa uwekezaji, kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa kuwa jengo la abiria litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka, jambo linalotarajiwa kuongeza uwezo wa Dodoma kupokea wageni wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa mnara wa kisasa wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, jengo la zimamoto la kiwango cha kimataifa, majengo ya kuzalisha umeme na jengo la hali ya hewa lenye vifaa vya kisasa vya usimamizi wa usafiri wa anga.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya (Mb) amesema kuwa, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati na ya kielelezo inayotekelezwa nchini chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema,mradi huo umebuniwa kwa mtazamo wa muda mrefu, ukiwa na uwezo wa kupanuliwa hatua kwa hatua kulingana na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga nchini.

“Uwanja huu umejengwa kwa viwango vya kisasa vya kimataifa na unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vya ndege vya kisasa zaidi nchini mara utakapoanza kutumika,” amesema Mhe.Kasekenya.
Amesisitiza kuwa,Serikali imejipanga kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili ahadi ya kuanza kwa shughuli za uwanja huo mwezi Septemba itimie, huku akibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya usafiri na kukuza uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji mkubwa wa kimkakati.

Katika Ziara hiyo Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar aliambatana na Naibu Mawaziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), Mhe. Laurent Luswetula, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour pamoja na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi wakiwemo Wakala wa Barabara nchini (Tanroads).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here