NA DIRAMAKINI
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza Klabu ya Young Africans (Yanga) faini ya Shilingi milioni 100 kwa kukiuka kanuni za Ligi Kuu baada ya wachezaji na benchi la ufundi kutotumia chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania, huku Rais wa klabu hiyo, Hersi Said na Afisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine wakipelekwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Maamuzi hayo yamefikiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB katika kikao chake kilichofanyika Julai 2, 2026, baada ya kupitia matukio mbalimbali yaliyojitokeza katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC na First League.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB leo, adhabu dhidi ya Yanga inatokana na wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi kutumia nyumba iliyopo nje ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, badala ya chumba rasmi cha kuvalia kilichotengwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kamati ilieleza kuwa,adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.
TPLB pia imeamua kuwapeleka Hersi Said na Andre Mtine katika Kamati ya Maadili ya TFF ili kutoa maelezo kuhusu tuhuma za ukiukaji wa mara kwa mara wa kanuni hiyo, ikieleza kuwa klabu hiyo tayari iliwahi kutozwa faini ya Shilingi milioni 30 mwezi Mei mwaka huu kwa kosa kama hilo.
Katika maamuzi mengine, Klabu ya KMC imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake watatu, Aimari Said Twalibu, Steven Donald Mgimwa na Hussein Ally Kihiyo, kuvaa jezi zenye namba zinazozidi 70 katika mchezo dhidi ya Simba SC, jambo lililokiuka Kanuni ya 17.2(2.5) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Aidha, Klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Shilingi milioni tano baada ya wachezaji na benchi lake la ufundi kutotumia chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo dhidi ya Namungo FC uliochezwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imechukua hatua kali dhidi ya Klabu ya Stand FC Masasi kufuatia kubainika kwa udanganyifu katika mchezo wa mchujo wa First League dhidi ya Pan African FC.
Mchezaji Ramadhani Bakari Mlaponi wa Lindi Soccer Academy amefungiwa kwa miezi 12 baada ya kubainika alitumia leseni ya mchezaji halali wa Stand FC, Swizani Edwini Matipani, ili kushiriki mchezo huo.
Kutokana na ukiukwaji huo, Stand FC imepoteza mchezo huo kwa mezani na Pan African FC imepewa ushindi wa mabao 3-0 kwa mujibu wa Kanuni ya 47(23) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Pia, kocha wa Stand FC, Mbano Kizito amefungiwa kwa miezi 12 na kutozwa faini ya Shilingi 500,000 baada ya kubainika alihusika kwa makusudi kumchezesha mchezaji ambaye hakuwa amesajiliwa na klabu hiyo.
TPLB imesema,hatua hizo zinalenga kulinda uadilifu wa mashindano na kuhakikisha klabu, viongozi, makocha na wachezaji wote wanazingatia kanuni na taratibu zinazosimamia ligi nchini.
