DODOMA-Wizara ya Fedha inawataarifu Wastaafu wote wanaoishi Wilayani waliopo kwenye Daftari la Pensheni, wanaolipwa pensheni ya kila mwezi na Wizara ya Fedha (HAZINA) kuwa Wizara inaendelea na awamu ya kwanza ya Zoezi la kugawa vitambulisho vipya vya wastaafu katika Wilaya zote Tanzania Bara kuanzia tarehe 06 Julai 2026 hadi 10 Julai 2026 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:30 jioni (Jumatatu hadi Ijumaa).
Ili kupata kitambulisho kipya, mstaafu anatakiwa kufika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya akiwa na Kitambulisho cha zamani cha mstaafu na Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Mstaafu ambaye hakujihakiki kati ya Januari 15 2026 hadi tarehe ya tangazo hili, anatakiwa ajihakiki kabla ya kwenda kuchukua Kitambulisho kipya.
Aidha, Tangazo hili haliwahusu wastaafu ambao wameshapokea Vitambulisho vipya kupitia Ofisi za Hazina Ndogo, Wastaafu waliostaafu kuanzia Julai, 2022, wanaolipwa pensheni na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na wale wanaolipwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Wastaafu wagonjwa wasioweza kufika katika Ofisi za Hazina Ndogo na Halmashauri za Wilaya watoe taarifa kwa Mkuu wa Hazina Ndogo katika mkoa husika au Mkurugenzi wa Wilaya anayoishi ili aweze kupelekewa Kitambulisho nyumbani kwake.
Wastaafu wote wanaarifiwa kuwa hakuna gharama yoyote ya kulipia huduma hii.
Limetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha.
