NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 22.6 za dawa za kulevya, lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya katika operesheni zilizofanyika nchini.

Ni kati ya Mei na Juni,2026 huku watuhumiwa 188 wakikamatwa na mali mbalimbali zinazohusishwa na biashara hiyo zikitaifishwa.
Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Julai 2,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusu operesheni hizo.
Amesema,operesheni hizo pia zimefanikisha kuteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi pamoja na tani 3.3 za bangi na mirungi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,katika operesheni hizo, DCEA ilikamata magari sita, bajaji mbili na pikipiki 33 zilizokuwa zikitumika kusafirisha dawa za kulevya, huku watuhumiwa wote wakichukuliwa hatua za kisheria.
Bidhaa zenye dawa tiba za kulevya zakamatwa Uwanja wa Ndege
Kamishina Lyimo amesema, moja ya mafanikio makubwa ya operesheni hizo ni ukamataji wa kilogramu 19.94 za bidhaa zilizokuwa zikisafirishwa zikitambulishwa kama virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) katika eneo la mizigo linalosafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Amesema,uchunguzi wa maabara uliofanywa ulibaini kuwa bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam, dawa inayotumika kutibu magonjwa kama wasiwasi, msongo wa mawazo na kukosa usingizi, lakini ambayo matumizi yake bila usimamizi wa daktari yanaweza kusababisha uraibu, kuathiri mfumo wa fahamu na kupumua, kupoteza fahamu na hata kifo.
Kwa mujibu wa DCEA, bidhaa hizo ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na zilikuwa zinaandaliwa kusafirishwa kwenda Barbados katika visiwa vya Karibiani.
Kufuatia tukio hilo, walikamatwa Agostino Metusela Ismaela (30) mkazi wa Kimara, Zamia Haridi Upunda (23) mkazi wa Bungoni Ilala na Habiba Ally Mziga (31) mkazi wa Mbezi Makonde.
Mirungi yafichwa kwenye matenga ya nyanya
Wakati huo huo, katika operesheni nyingine iliyofanyika eneo la Manyanya wilayani Kinondoni, DCEA ilikamata kilogramu 34.87 za mirungi zilizokuwa zimefichwa kwa kuchanganywa na matenga ya nyanya ndani ya gari aina ya Fuso lililotoka Tarakea mkoani Kilimanjaro.
Kamishina Jenerali Lyimo amesema,mzigo huo uliingizwa nchini kutoka Kenya na baada ya kufikishwa Dar es Salaam ulianza kusambazwa kwa kutumia bajaji.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Mohamed Omary Mohamed (24) mkazi wa Tandale, Suleman Omary Sujuti (34), dereva wa gari hilo kutoka Tarakea wilayani Rombo pamoja na Deo Paschal Maratua (32) dereva wa bajaji na mkazi wa Tandale kwa Mtogole.
Aidha, DCEA inaendelea kumtafuta Husseini Jumaa Salimu (52) anayedaiwa kuwa nchini Kenya, kwa tuhuma za kuhusika na mtandao huo wa usafirishaji wa mirungi.
Vinywaji vyenye THC vyanaswa sokoni
Katika operesheni ya pamoja iliyoshirikisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), DCEA ilifanya ukaguzi katika duka la Village Supermarket jijini Dar es Salaam na kubaini vinywaji aina ya energy drinks vyenye kemikali ya THC, ambayo ni kiambata kinachopatikana kwenye bangi.
Amesema,jumla ya makopo 122 yenye ujazo wa mililita 250 kila moja, sawa na lita 30.5 za kinywaji chenye chapa ya TRIP yalikamatwa.
Katika tukio hilo walikamatwa Syed Abdul Bast (43) raia wa Pakistan pamoja na Dhirendra Kumar Gorodhan (45), Mtanzania mwenye asili ya Asia.Kamishina Jenerali Lyimo amesema,THC inaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuamsha magonjwa ya akili, kuathiri mfumo wa fahamu, kuongeza uwezekano wa vitendo vya uhalifu na kuchochea matumizi ya dawa nyingine za kulevya.
Ukamataji waendelea mikoani
Operesheni nyingine zilizofanyika katika Bandari ndogo ya boti kati ya Dar es Salaam na Zanzibar zimefanikisha kukamatwa kwa gramu 972.05 za mirungi zilizokuwa zinasafirishwa na raia wa Kenya, Kalsam Abdurahaman Sebbi (43) mwenye makazi yake Mombasa.
Kamisha Jenerali Lyimo pia amesema,wilayani Kigamboni, DCEA ilikamata gramu 162.48 za heroin na kumkamata mtuhumiwa Omary Miraji Mboaneani.
Mkoani Arusha, kilogramu 106.04 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Premio huku mtuhumiwa Goodluck Erasto Nyakasesela (35) ambaye ni mtaalamu wa picha za kitabibu (Radiographer) katika Hospitali ya Ocean Road akikamatwa.
Wilayani Same mkoani Kilimanjaro, kilogramu 240 za mirungi zilizokuwa zimefichwa ndani ya mabegi ya nguo zilikamatwa, huku Irene Obedi Sule na Elissa Obedi Sule wakitiwa mbaroni.
Kwa mujibu wa DCEA, operesheni zilizofanyika katika mikoa mingine nchini ziliwezesha kukamatwa kwa tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 40 za skanka na gramu 11.63 za heroin.
Aidha, tani 3.3 za bangi na mirungi pamoja na ekari 228.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika wilaya za Chamwino (Dodoma), Kilwa (Lindi), Songerema na Geita.
Ushirikiano wa kimataifa waimarishwa
Kamishina Jenerali Lyimo amesema,uchunguzi wa pamoja uliofanywa kwa kushirikiana na mamlaka za Eswatini, Afrika Kusini, Msumbiji na Zambia umebaini kuwepo kwa baadhi ya raia wa Tanzania wanaohusishwa na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya waliokimbilia katika nchi hizo.
Amesema,DCEA itaendelea kushirikiana na mamlaka za nchi hizo kufanya operesheni za pamoja kwa lengo la kuwakamata wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Kamishina Jenerali Lyimo amesema,mamlaka imeimarisha ushirikiano na taasisi za udhibiti nchini ili kukabiliana na mbinu mpya zinazotumiwa kusafirisha dawa za kulevya kupitia virutubisho vya lishe, dawa na kemikali, kwa kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kufanya ukaguzi na kuendesha operesheni za pamoja kwa lengo la kulinda afya, usalama na ustawi wa jamii.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Operesheni Kabambe
























