DCEA yakamata virutubisho vyenye dawa ya kulevya vilivyokuwa vikisafirishwa kwenda Barbados

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 19.94 za bidhaa zilizoingizwa nchini kama virutubisho vya lishe,lakini ikabainika kuwa zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam, huku watu watatu wakikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 2,2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,ukamataji huo ulifanyika katika operesheni za kudhibiti dawa za kulevya zilizotekelezwa nchini kati ya Mei na Juni,mwaka huu.

Amesema,bidhaa hizo zilizotambulishwa kama virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) zilikamatwa katika eneo la mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

"Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maabara, ilibainika kuwa bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Kwa mujibu wa DCEA, bidhaa hizo ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na zilikuwa zinaandaliwa kusafirishwa kwenda Barbados katika visiwa vya Karibiani.

Kufuatia tukio hilo, DCEA imewakamata Agostino Metusela Ismaela (30) mkazi wa Kimara,Zamia Haridi Upunda (23) mkazi wa Bungoni, Ilala na Habiba Ally Mziga (31) mkazi wa Mbezi Makonde ambao wanashikiliwa kwa hatua za kisheria.

Amefafanua kuwa,Prazepam ni dawa tiba yenye asili ya kulevya iliyopo katika kundi la benzodiazepine, inayotumika kutibu matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo wasiwasi, msongo wa mawazo na kukosa usingizi.
Hata hivyo, ameonya kuwa matumizi ya dawa hiyo bila ushauri au maelekezo ya daktari yanaweza kusababisha uraibu, kuathiri mfumo wa fahamu na mfumo wa upumuaji, kupoteza fahamu na hata kusababisha kifo.

Amesema,DCEA itaendelea kuimarisha ukaguzi katika mipaka, viwanja vya ndege na maeneo mengine ya usafirishaji wa mizigo ili kudhibiti mbinu mpya zinazotumiwa na mitandao ya biashara ya dawa za kulevya kuingiza au kusafirisha bidhaa zenye viambata vya dawa hizo nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here