NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema,inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kuelimisha umma kuhusu madhara ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya, huku ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana nao katika kukabiliana na mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu wa dawa hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 3,2026 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa DCEA,Bi.Florence Khambi wakati akizungumza katika semina ya siku moja ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Bi. Khambi amesema,ushirikiano uliopo kati ya DCEA na vyombo vya habari umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na biashara hiyo haramu.
Ameeleza kuwa,wahalifu wa dawa za kulevya wanaendelea kubuni mbinu mpya za kushawishi watumiaji, kusafirisha, kuzalisha na kusambaza dawa hizo ikiwemo matumizi mabaya ya kemikali bashirifu ili kukwepa mifumo ya udhibiti na uchunguzi wa mamlaka husika.
"Wahalifu wa dawa za kulevya hubuni mbinu mpya kila siku.Ndiyo maana tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kushirikiana na ninyi waandishi wa habari kwa kuwapa elimu kuhusu kemikali bashirifu na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu hao ili muwe na uelewa wa kutosha na muweze kuielimisha jamii kupitia kalamu zenu."
Ameongeza kuwa,semina hiyo imelenga kuziba pengo la uelewa kuhusu masuala ya dawa za kulevya na kuwajengea waandishi uwezo wa kuandika habari zenye usahihi na zinazosaidia jamii kutambua athari za tatizo hilo.
Katika mafunzo hayo, washiriki wamepata elimu kutoka kwa wataalamu wa DCEA kuhusu dawa tiba zenye asili ya kulevya, kemikali bashirifu, aina mpya za dawa za kulevya pamoja na mbinu zinazotumiwa katika uendeshaji wa maabara bubu za kutengeneza dawa hizo.
Aidha, waandishi hao wameelimishwa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa afya, usalama wa jamii na maendeleo ya Taifa, pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuhamasisha mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.
DCEA imesisitiza kuwa,ushirikiano kati ya mamlaka hiyo, vyombo vya habari na wananchi ni nyenzo muhimu katika kuzuia kuenea kwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, hasa wakati ambapo wahalifu wanaendelea kubadilisha mbinu zao ili kukwepa mkono wa sheria.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)










