NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeongeza Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi asilimia 6.25 kwa robo tatu ya mwaka inayoishia Septemba,2026 hatua inayolenga kudhibiti ongezeko la mfumuko wa bei linalochochewa na kupanda kwa bei za mafuta,mbolea na gharama za usafirishaji duniani.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha kamati kilichofanyika Julai 2,2026 ambapo ilielezwa kuwa,ongezeko la riba litasaidia kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 bila kuathiri ukuaji wa uchumi.
Katika tamko lililotolewa na Mwenyekiti wa MPC ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel M. Tutuba leo Julai 3,2026 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam,kamati imeeleza kuwa, shinikizo la mfumuko wa bei limeongezeka kutokana na athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, ambao umechangia kupanda kwa bei za mafuta ghafi,mbolea na gharama za usafirishaji katika masoko ya dunia.
Hata hivyo, kamati imeeleza kuwa matarajio ya mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2025/26 yanatarajiwa kushusha bei za vyakula,huku kuongezeka kwa mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu,mazao ya kilimo na utalii kukiisaidia shilingi kuendelea kuwa imara.
Amesema,hali hiyo itachangia kupunguza gharama za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei katika nusu ya pili ya mwaka 2026.
Vilevile,kamati imebainisha kuwa,ukuaji wa uchumi wa dunia ulipungua katika robo mwaka iliyoishia Juni,2026 kutokana na kuongezeka kwa athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati, uliovuruga usambazaji wa mafuta na njia muhimu za biashara.
Hali hiyo imeongeza mfumuko wa bei duniani na kupunguza matarajio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2026.
Licha ya changamoto hizo za kimataifa, MPC imesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha uimara.
Kwa Tanzania Bara, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 6 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, ukichochewa na sekta za kilimo, ujenzi, madini, huduma za kifedha na usafirishaji.
Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.6, ukichangiwa zaidi na sekta za utalii na ujenzi.
Gavana Tutuba ameeleza kuwa,katika nusu ya pili ya mwaka huu, uchumi unatarajiwa kuendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 6.
Mfumuko wa bei wabaki ndani ya lengo
Kwa upande wa mfumuko wa bei, kamati imesema Tanzania Bara uliongezeka hadi asilimia 4.2 mwezi Mei 2026 kutoka asilimia 3.2 mwezi Machi, lakini uliendelea kubaki ndani ya lengo la Benki Kuu la asilimia 3 hadi 5.
Aidha, ruzuku ya mafuta iliyotolewa na Serikali katika miezi ya Mei na Juni ilisaidia kupunguza kasi ya ongezeko hilo.
Kwa Zanzibar, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 5.5 mwezi Mei kutoka asilimia 4.9 mwezi Machi, huku ukitarajiwa kurejea ndani ya kiwango kinacholengwa kadri athari za nje zitakavyopungua.
Wakati huo huo,kamati pia imeeleza kuwa,hali ya ukwasi nchini iliendelea kuwa tulivu katika robo ya pili ya mwaka 2026, huku mikopo kwa sekta binafsi ikikua kwa wastani wa asilimia 24 kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji.
Sekta ya benki pia iliendelea kuwa imara, yenye faida na mtaji wa kutosha kukabiliana na misukosuko ya kifedha, huku kiwango cha mikopo chechefu kikibaki asilimia 2.9 mwezi Mei 2026, chini ya kiwango cha juu kinachokubalika cha asilimia 5.
Benki Kuu imrsema,akiba ya fedha za kigeni imefikia takribani dola za Marekani bilioni 6, kiwango kinachotosheleza kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.3, juu ya lengo la taifa la angalau miezi minne.
Aidha, akiba hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani.
Kwa upande wa mapato ya Serikali, kamati imeeleza kuwa,ukusanyaji wa kodi umeendelea kufanya vizuri, huku mapato ya ndani yakitarajiwa kufikia asilimia 16.8 ya Pato la Taifa katika mwaka wa fedha 2025/26, kutoka asilimia 15.6 mwaka uliotangulia.
Hata hivyo,Kamati ya Sera ya Fedha imesema, itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia pamoja na vihatarishi vinavyoweza kuongeza mfumuko wa bei, huku kikao kijacho cha kutangaza Riba ya Benki Kuu kikitarajiwa kufanyika Oktoba 7, 2026.
