HARARE-Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Leo Julai 1, 2026, amepatiwa taarifa ya kina kuhusu maazimio na mapendekezo yaliyofikiwa na vikao vya Makatibu Wakuu wa Hazina, Makatibu Wakuu wa Afya na Maafisa Waandamizi wa Benki Kuu za SADC, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa Ngazi ya Mawaziri unaotarajiwa kufanyika Julai 2, 2026, mjini Harare, Zimbabwe.
Taarifa hiyo iliwasilishwa katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, kikilenga kuwawezesha Mawaziri kupitia kwa kina ajenda na mapendekezo yatakayowasilishwa kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi ya Kisera katika kikao cha Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa SADC.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mb), Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Mhe. Ally Hassan Omar King (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. CP Suzan Kaganda, pamoja na wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki mkutano huo.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alisema mapendekezo yaliyowasilishwa yanatokana na majadiliano ya kina yaliyofanywa katika vikao vya Makatibu Wakuu wa Hazina na yanahusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano wa kifedha na uwekezaji ndani ya SADC.
Alieleza kuwa ajenda hizo zinajumuisha hatua za kuimarisha usimamizi wa uchumi wa kikanda, uhamasishaji wa rasilimali fedha za maendeleo, utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kikanda, maendeleo ya sekta ya fedha, pamoja na maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji katika nchi wanachama wa SADC.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Luswetula aliushukuru ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kwa maandalizi madhubuti na taarifa ya kina iliyowasilishwa, akieleza kuwa itaiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika mijadala ya Mawaziri na kutoa mchango wenye tija katika maamuzi yatakayochukuliwa kwa manufaa ya ukanda wa SADC.
Alisisitiza kuwa maandalizi hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya Tanzania ya kuendelea kutekeleza kikamilifu wajibu wake ndani ya SADC na kuchangia juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kifedha, uwekezaji na maendeleo endelevu ya nchi wanachama.
Awali, ujumbe wa Tanzania ulipokelewa na kukaribishwa katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. CP Suzan Kaganda, ambaye aliwapongeza wajumbe kwa kuwakilisha vyema Taifa katika mkutano huo muhimu wa kikanda.
Mhe. Balozi Kaganda alieleza kuwa Ubalozi utaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unakuwa wenye mafanikio.
Vilevile, Mhe. Balozi Kaganda alisisitiza kwa watanzania kwa nyadhifa zao mbalimbali kuendelea kuitangaza Tanzania kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini kwa manufaa ya Taifa kwa vile kuna vitu/fursa nyingi zilizopo nchini lakini watu wengi hawazitambui kwa vile hazitangazwi kwa umma.
Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa SADC unatarajiwa kufanyika Julai 2, 2026, ambapo Mawaziri watajadili na kufanya maamuzi kuhusu mapendekezo yaliyowasilishwa na Makatibu Wakuu wa Hazina, Afya na Maafisa Waandamizi wa Benki Kuu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kifedha, uwekezaji na maendeleo endelevu katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.






