MANYARA-Juni 30,2026 imefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi namba 14623/2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbulu, Mheshimiwa Vitus Kapugi dhidi ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamusta,Bw. Daniel Gidambisye Murayda na Mhasibu Bw. James Cosmas Basil.
Washtakiwa wanashtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya 2022 ikisomwa pamoja na aya ya 21 Jedwali la kwanza na vifungu vya 57 (1) na 61 (2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, pamoja na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200] marejeo ya 2022.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Bw.Amiri Addy ameieleza mahakama kuwa,watuhumiwa walimpa mzabuni kazi ya kusambaza vifaa na ujenzi katika mradi wa "WATER SANITAZATION PROJECT" Shule ya Msingi Nyamusta bila kushindanisha zabuni na hivyo kukiuka kanuni namba 164 na 203 za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2023.
Washtakiwa wamesomewa hati ya mashtaka na wote wawili wamekana kutenda makosa hayo.
Aidha,washtakiwa wametimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mtuhumiwa na kusaini bondi ya shilingi 5,000,000 na kwa sasa wapo nje kwa dhamana.
Shauri limehairishwa hadi Julai 14,2026 kwa ajili ya Hoja za awali (PH).
