Wananchi waipongeza NHC kwa miradi bora ya makazi,waibua mapendekezo ya kuwafikia zaidi wenye vipato vya chini

NA GODFREY NNKO

WANANCHI mbalimbali jijini Dar es Salaam wamepongeza juhudi za Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya makazi, wakisema imeendelea kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwapatia makazi bora, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mchango wa shirika hilo katika mapato ya Serikali.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bi. Domina Rwemanyila akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu shirika kwa wananchi waliotembelea banda la NHC katika Maonesho ya Sabasaba 2026.

Pongezi hizo wamezitoa leo Julai 1,2026 walipotembelea banda la NHC katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Mbali na kutembelea banda hilo, wananchi hao wamepata elimu kuhusu majukumu ya shirika, miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa nchini, pamoja na taratibu za kununua na kupanga nyumba zinazomilikiwa na NHC.
Baadhi ya wananchi hao, akiwemo Erasto Golan na Elias George wamesema,ziara yao katika banda la NHC imewapa uelewa mpana kuhusu shughuli za shirika hilo na kuwasaidia kubaini ukweli kuhusu huduma zake, tofauti na taarifa walizokuwa wakizisikia awali.

Wamesema kabla ya kupata elimu hiyo walikuwa wakiamini taarifa zilizosambaa katika jamii kwamba nyumba za NHC hupangwa kwa watu wachache wenye uwezo mkubwa wa kifedha, jambo ambalo sasa wamebaini kuwa halina ukweli.

"Baada ya kupata maelezo kutoka kwa maafisa wa NHC, tumeona kuwa kila Mtanzania anayekidhi masharti ana nafasi ya kuomba na kupanga nyumba za shirika kwa kufuata taratibu zilizowekwa, ikiwemo kujaza fomu maalumu za maombi. Taarifa tulizokuwa tunazisikia hazikuwa sahihi,"amesema Golan.

Wameeleza kuwa,mfumo wa upangishaji wa nyumba unaotumiwa na NHC ni wa wazi, shirikishi na unaowapa fursa wananchi wote bila ubaguzi, huku wakibainisha kuwa gharama za upangishaji ni nafuu kulingana na maeneo husika.

Kutokana na elimu waliyoipata, wananchi hao wamesema wako tayari kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuhusu huduma zinazotolewa na NHC, ikiwemo fursa za kupanga au kununua nyumba za kisasa zinazojengwa na shirika hilo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Alex Chonya amesema NHC limeendelea kuthibitisha nafasi yake kama taasisi muhimu katika sekta ya makazi nchini kupitia utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, amependekeza shirika hilo liendelee kuboresha mikakati yake ya uwekezaji kwa kujenga nyumba nyingi zaidi zinazolenga wananchi wa kipato cha chini ili kuwapa nafasi ya kumiliki makazi bora.

Amesema,hatua hiyo itaongeza idadi ya Watanzania wanaoweza kumiliki nyumba huku ikichochea ustawi wa jamii na maendeleo ya sekta ya makazi nchini.

Akitoa mfano, amesema utaratibu unaotumiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wa kuweka viwango maalumu vya ada vinavyowapa nafuu Watanzania umetengeneza hamasa kubwa ya kutembelea hifadhi za taifa.

"Hivyo na NHC likitenga miradi yenye bei rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini, watu wengi zaidi wataweza kununua nyumba na kufikia ndoto ya kumiliki makazi bora,"amesema.

Naye Aisha Juma mkazi wa Temeke amesema, mafanikio ya NHC ni mafanikio ya Watanzania wote kutokana na mchango wake katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

Amesema,shirika hilo limeendelea kuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa taasisi za umma kwa jinsi linavyotekeleza miradi ya maendeleo, sambamba na kuchangia mapato ya Serikali kupitia gawio.
"Jana tuliona Ikulu Magogoni viongozi wa NHC wakikabidhi Serikali gawio la mabilioni ya shilingi. Fedha hizo ni muhimu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha Watanzania. Hili linastahili pongezi," alisema.

NHC ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yaliyoanza Juni 28, 2026 yakibeba kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa 'SabaSaba' Fahari ya Tanzania."

Kupitia maonesho hayo, maafisa wa shirika wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya NHC, miradi ya makazi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na fursa zilizopo za kununua na kupanga nyumba zinazomilikiwa na shirika hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here