NA GODFREY NNKO
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu amesema, Bunge linatarajia kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa chimbuko lake mwaka 1926, huku kilele cha maadhimisho hayo kikitarajiwa kufanyika Januari 27,2027.
Spika Zungu ametoa taarifa hiyo leo Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam alipokutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa lengo la kuelezea maandalizi ya maadhimisho hayo ya kihistoria.
Amesema,mwaka huu unaweka alama muhimu katika historia ya Taifa kutokana na kutimia kwa karne moja tangu kuanzishwa kwa mhimili huo ambao umeendelea kuwa nguzo ya demokrasia nchini kupitia majukumu yake ya kutunga sheria, kuwakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.
Kwa mujibu wa Spika huyo, maadhimisho hayo yataongozwa na kaulimbiu isemayo "Miaka 100 ya Bunge: Historia Yetu, Dira Yetu," yakilenga kutoa fursa ya kutafakari historia ya Bunge, kuthamini mchango wa viongozi waliowahi kulitumikia kwa nyakati mbalimbali, pamoja na kuweka mwelekeo wa maendeleo ya mhimili huo kwa karne ijayo.
Ameeleza kuwa,maadhimisho hayo yataonesha safari ya miaka 100 ya maendeleo ya Bunge la Tanzania, kuanzia kuanzishwa kwa Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1926 wakati Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza, hadi kufikia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Spika Zungu amesema,chimbuko la Bunge linaanzia Machi 19,1926 wakati Tanganyika ikiwa koloni la Uingereza, ambapo Baraza la Kutunga Sheria lilianzishwa kabla ya kuzinduliwa rasmi Oktoba 10,1926 na kuanza shughuli zake mwezi Desemba,mwaka huo.
Ameongeza kuwa,historia ya taasisi hiyo imepitia hatua mbalimbali muhimu, ikiwemo kipindi cha Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 na baadaye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 uliounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, amesema maandalizi ya maadhimisho hayo yanajumuisha shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika kipindi chote kuelekea kilele cha sherehe hizo Januari 2027, zikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuelewa historia, mchango na nafasi ya Bunge katika ujenzi wa Taifa.
Katika mkutano huo, Spika Zungu amevitaka vyombo vya habari kushiriki kikamilifu kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu maadhimisho hayo ili historia ya Bunge la Tanzania iendelee kuhifadhiwa na kufahamika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
"Ninyi wanahabari ni wadau muhimu katika kuandika historia ya Taifa letu. Tunatarajia ushiriki wenu mkubwa kuhakikisha Watanzania na dunia kwa ujumla wanafahamu historia ya miaka 100 ya Bunge letu."
Mbali na maadhimisho hayo, Spika Zungu amewataka Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha umoja, mshikamano na amani, akisisitiza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya Taifa.
Amesema,maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana kupitia migogoro, chuki au maandamano yenye kuleta taharuki, bali kupitia maridhiano, mazungumzo na ushirikiano wa wananchi wote.
"Nchi haiwezi kujengwa kwa maandamano wala kwa watu kushutumiana. Amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani, hivyo tunapaswa kuilinda na kuithamini wakati wote,"amesema Mheshimiwa Zungu.
Spika Zungu pia ameeleza kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha demokrasia, utawala bora na maridhiano ya kisiasa, ikiwemo kuweka mazingira yaliyowezesha baadhi ya wanasiasa waliokuwa nje ya nchi kurejea Tanzania.
Ameongeza kuwa,pamoja na hatua hizo, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo miundombinu, huduma za jamii na mageuzi ya kidemokrasia, ambayo amesema yanastahili kutambuliwa kwa mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Tags
Bunge la Tanzania
Habari
Miaka 100 ya Bunge la Tanzania
Mussa Azzan Zungu
Spika Mussa Azzan Zungu

