Waziri wa Fedha,Balozi Omar na Waziri Dkt.Kijaji wajadili mikakati ya kukuza utalii kufikia malengo ya Dira 2050

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya kikao na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Utalii na Maliasili, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuendeleza na kukuza sekta ya utalii na maliasili ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano yatakayowezesha kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza mapato yatokanayo na utalii na maliasili, pamoja na kuboresha mifumo na sera zinazochochea ukuaji endelevu wa sekta hizo.
Aidha, walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara hizo mbili katika kutekeleza vipaumbele vya Serikali.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha uratibu wa kisekta na kuoanisha mikakati ya maendeleo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kupitia ushirikiano huo, Serikali inalenga kuongeza mchango wa sekta ya utalii na maliasili katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayokusudia kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa thamani ya dola za Marekani Trilioni 1.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Bw. Musa Nassoro Kuji, Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Bw. Mlage Yussuf Kabange na Maafisa wengine Waandamizi wa Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here