TANGA-Wananchi wa Kijiji cha Hamboyo, Kata ya Manolo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wamehimizwa kuwa wazalendo, kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuendelea kushiriki kikamilifu katika ulinzi na usalama wa maeneo yao.
Elimu hiyo imetolewa na Polisi Kata ya Manolo, Inspekta wa Polisi (INSP) Reagan Mtenga, wakati akishiriki na wananchi hao katika ujenzi wa Shule ya Msingi ya kijiji hicho, ambapo pia alitoa elimu kuhusu uzalendo, ulinzi shirikishi na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
INSP Mtenga amewataka wananchi hao kuwa wazalendo kwa kuitunza amani iliyopo na kujitolea katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuwa ni kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.
Aidha, amewataka kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu vitendo vya uhalifu na wahalifu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Pamoja na hayo, amewahimiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, hususan dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kutoa taarifa mapema pale wanapobaini vitendo hivyo.






