Rais Dkt.Samia ampongeza Hawa Wanyeche kwa kutwaa Ubingwa wa Uganda Ladies Open

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza mchezaji wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Hawa Wanyeche kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Uganda Ladies Open, akisema ushindi huo ni fahari kwa Taifa na ishara ya uwezo wa wanamichezo wa Tanzania kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Ametoa pongezi hizo kufuatia ushindi wa Wanyeche katika mashindano hayo yaliyowakutanisha wachezaji kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Ghana, Japan, Kenya, Nigeria, Rwanda, Tanzania na wenyeji Uganda.

Katika pongezi zake, Rais Samia amesema, mafanikio hayo yanaonesha kuwa,Tanzania ina vipaji na uwezo mkubwa katika mchezo wa gofu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaunga mkono wanamichezo wanaoliwakilisha Taifa katika mashindano ya kimataifa.

“Ninampongeza Hawa Wanyeche, mchezaji wa Klabu ya Gofu ya Lugalo,kwa kutwaa ubingwa wa Uganda Ladies Open, mashindano yaliyokutanisha wachezaji kutoka Ghana, Japan, Kenya, Nigeria, Rwanda, Tanzania na Uganda,”amesema Rais Dkt.Samia.

Amesema,ushindi huo ni “fahari kubwa kwa Taifa letu”, kwa kuwa unaonesha uwezo wa wachezaji wa Tanzania kushindana na kufanya vizuri katika majukwaa ya kimataifa.

Rais Dkt.Samia amesema, mafanikio ya Wanyeche yanapaswa kuwa chachu ya kuendelea kuwekeza katika michezo, kuibua vipaji vipya na kuwaandaa wanamichezo kushiriki katika mashindano ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Aidha, Rais Samia amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya michezo nchini kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanamichezo katika taaluma mbalimbali.

“Serikali itaendelea kuimarisha na kuendeleza michezo nchini kwa kuweka mazingira bora kwa wanamichezo wote, pamoja na kuwawezesha kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa,”amesema.

Ushindi wa Wanyeche unaongeza sura mpya katika mafanikio ya Tanzania katika mchezo wa gofu, huku ukitoa hamasa kwa wachezaji wengine nchini kuendelea kujituma na kutumia fursa za mashindano ya kimataifa kuonyesha uwezo wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here