NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),Félix Tshisekedi amelikabidhi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) magari 10 mapya aina ya Toyota Land Cruiser utility pickup kwa ajili ya kuimarisha operesheni za pamoja dhidi ya kundi la kigaidi la Allied Democratic Forces (ADF) Mashariki mwa DRC.
Magari hayo yamekabidhiwa kwa UPDF chini ya Operesheni Shujaa, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa jeshi hilo katika mapambano dhidi ya ADF na jitihada za kurejesha amani na usalama wa kudumu katika maeneo yaliyoathiriwa na vitendo vya kundi hilo.
Akikabidhi magari hayo kwa niaba ya Rais Tshisekedi, Gavana wa Kivu Kaskazini, Meja Jenerali Somo Kakule Evariste amesema,Rais huyo anatambua na kuthamini ushirikiano imara uliopo kati ya Serikali za DRC na Uganda, pamoja na mafanikio yaliyopatikana kupitia operesheni za kijeshi za pamoja dhidi ya ADF.
Amesema, magari hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa vikosi vinavyoshiriki katika Operesheni Shujaa, hasa katika usafirishaji wa askari na vifaa na kurahisisha utekelezaji wa majukumu katika maeneo yenye changamoto za kiusalama.
Kwa upande wake, Gavana wa Ituri amezipongeza FARDC na UPDF kwa ushirikiano wao katika operesheni hizo, akisema juhudi za pamoja zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya amani na utulivu mashariki mwa DRC.
UPDF yaahidi kuendelea kuwasaka ADF
Akizungumza wakati akipokea magari hayo mjini Beni, Kamanda wa Kikosi Kazi cha Pamoja cha Operesheni Shujaa na Kamanda wa Divisheni ya UPDF ya Mountain Infantry, Meja Jenerali Stephen Mugerwa amemshukuru Rais Tshisekedi kwa msaada huo.
Mugerwa amesisitiza dhamira ya vikosi vya pamoja kuendelea kuwafuatilia wapiganaji wa ADF hadi pale kundi hilo litakaposhindwa kabisa na kutokuwa na uwezo wa kuendelea kutishia usalama wa wananchi.
Operesheni Shujaa ilianzishwa Novemba 2021 na imehusisha vikosi vya UPDF na Jeshi la DRC (FARDC) katika mapambano dhidi ya ADF katika maeneo ya Kivu na Ituri.
Operesheni imeleta mabadiliko Mashariki mwa DRC
Tangu kuanzishwa kwake, Operesheni Shujaa imeripotiwa kupata mafanikio mbalimbali katika kurejesha usalama katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa DRC.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuwawezesha maelfu ya watu waliokuwa wameyakimbia makazi yao kurejea nyumbani, kuwaokoa watu waliotekwa nyara, kupunguza uwezo wa ADF kufanya operesheni na kuwaondoa baadhi ya makamanda wake wakuu.
Aidha, kuimarika kwa usalama pia kumewezesha shule kufunguliwa tena katika baadhi ya maeneo, huku biashara ya mipakani kati ya Uganda na DRC ikiongezeka.
Pia,hali hiyo imeambatana na maendeleo katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, ikiwemo Beni–Kasindi, Beni–Biakato, Biakato–Mangina na Luna–Komanda, ambayo imeendelea kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu kati ya maeneo hayo.
Biashara ya mipakani yaongezeka
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na UPDF, maboresho ya usalama na miundombinu yamechangia ongezeko kubwa la biashara kati ya Uganda na DRC.
Idadi ya malori ya mizigo yanayovuka mpaka kati ya nchi hizo imeongezeka kutoka takribani malori 13,000 kwa mwezi hadi zaidi ya 30,000, jambo linaloashiria kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na usafirishaji katika eneo hilo.
Operesheni Shujaa ilianzishwa baada ya mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Kampala, Uganda, na baadaye mazungumzo kati ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Tshisekedi yakapelekea kuanzishwa kwa operesheni hiyo ya pamoja.
Tangu wakati huo, operesheni hiyo imekuwa sehemu muhimu ya ushirikiano wa kiusalama kati ya Uganda na DRC, huku ikiendelea kulenga kupunguza na hatimaye kuondoa uwepo wa ADF katika maeneo ya mashariki mwa DRC.
Kwa hatua ya Rais Tshisekedi kukabidhi UPDF magari hayo, ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili unaonekana kuendelea kupewa uzito katika juhudi za kukabiliana na ugaidi na kurejesha mazingira yatakayowezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani.(UPDF)


