DODOMA-Wananchi mbalimbali jijini Dodoma wametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofungwa rasmi Agosti 8, 2026, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maonesho hayo yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti 2026, yameongozwa na kaulimbiu “Tambua Soko; Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050.”Kupitia banda lake, Benki Kuu ilitoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya msingi katika kukuza na kudumisha uthabiti wa uchumi wa Taifa.
Elimu hiyo ilijikita katika maeneo mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Fedha, kudumisha uthabiti wa bei, kusimamia sekta ya fedha na mifumo ya malipo, pamoja na kuhamasisha matumizi ya huduma rasmi za fedha kwa manufaa ya wananchi na uchumi kwa ujumla.
Katika kipindi chote cha maonesho, banda la Benki Kuu lilitembelewa na wananchi kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo viongozi wa Serikali, wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi, wanafunzi na wadau wengine.
Wageni waliotembelea banda hilo walipata fursa ya kujifunza kuhusu majukumu na shughuli mbalimbali za Benki Kuu, kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa BoT.






