MBEYA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepata ushindi wa kwanza katika Kundi la Mamlaka za Udhibiti katika Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) 2026, yaliyofanyika katika kanda mbalimbali nchini kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti,2026.
Katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Tawi la Benki Kuu ya Tanzania Mbeya liliibuka mshindi wa kwanza katika Kundi la Mamlaka za Udhibiti.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, na kupokelewa na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mbeya, Dkt. James Machemba.
Kwa upande wa Kanda ya Kusini, Tawi la BoT Mtwara nalo lilipata ushindi wa kwanza katika kundi hilo. Tuzo hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, na kupokelewa na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mtwara, Bw. Moto Lubogi.Katika Kanda ya Kaskazini, Tawi la BoT Arusha lilitwaa tuzo ya ushindi wa kwanza katika Kundi la Mamlaka za Udhibiti. Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla, na kupokelewa na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Arusha, Dkt. Charles Masenya.
Aidha, katika Kanda ya Ziwa, Tawi la BoT Mwanza lilipewa tuzo maalum ya udhamini. Tuzo hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mohamed Mtanda, na kupokelewa kwa niaba ya Tawi na Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Bw. Johnas Ezekiel.
Mafanikio hayo yanaakisi juhudi za Benki Kuu katika kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya fedha na uchumi, sambamba na kushiriki kikamilifu katika majukwaa yanayowakutanisha wananchi, taasisi za umma na wadau mbalimbali.







