ARUSHA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha programu ya kuhamasisha umuhimu wa uwasilishaji wa taarifa za mikopo kwa mabenki, watoa huduma ndogo za kifedha na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Programu hiyo imefanyika kuanzia tarehe 21 hadi 25 Septemba 2026 katika Ofisi ya Tawi la Benki Kuu ya Tanzania Arusha, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa wadau kuhusu umuhimu wa mfumo wa taarifa za mikopo, pamoja na kuimarisha ubora, usahihi, ukamilifu na uwasilishaji wa taarifa za mikopo kwa wakati katika mfumo wa Benki Kuu.
Programu hiyo imeandaliwa kufuatia kubainika kwa baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa mfumo wa taarifa za mikopo, ikiwemo kuchelewa kwa baadhi ya watoa taarifa kuwasilisha taarifa kuhusu mikataba ya mikopo iliyofungwa.
Kuchelewa kwa taarifa hizo kunaweza kusababisha kuwepo kwa taarifa zilizopitwa na wakati katika mfumo wa taarifa za mikopo na, kwa upande mwingine, kuibua malalamiko kutoka kwa wateja.
Aidha, imebainika kuwa baadhi ya watoa huduma ndogo za kifedha wamekuwa na kiwango cha chini cha uwasilishaji wa taarifa za mikopo.
Akizungumza wakati wa programu hiyo, Dkt. Hapho Hoha, kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, alisema programu hiyo inalenga kuwajengea uwezo washiriki na kuongeza uelewa wao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mfumo wa taarifa za mikopo.
Alisema washiriki wanapatiwa elimu kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia taarifa za mikopo; muundo na namna sahihi ya kuwasilisha taarifa; taratibu za uwasilishaji na marekebisho ya taarifa zilizokataliwa.
Pia,matumizi ya taarifa za mikopo katika tathmini ya maombi ya mikopo; pamoja na taratibu za kushughulikia malalamiko yanayohusiana na taarifa za mikopo.
Aidha, programu hiyo inawapa washiriki fursa ya kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya taarifa za mikopo katika kusaidia kufanya maamuzi sahihi ya utoaji wa mikopo, kuimarisha usimamizi wa mikopo na kuongeza uwajibikaji miongoni mwa wadau wa sekta ya fedha.
Katika kuimarisha uelewa na matumizi ya mfumo huo, washiriki pia wanapata fursa ya kupata taarifa zao za mikopo bila malipo, ikiwa ni sehemu ya programu hiyo.


